HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 07, 2020

HDIF, COSTECH kukutanisha wabunifu mikoa mitano

 Mkurugenzi Mkazi wa HDIF Joseph Manirakiza (kulia), akizungumzia wiki ya ubunifu itakayoanza Machi 8,2020 katikati ni Mkuu wa DFID, Natalie Smith na kushoto ni Mkurugenzi wa COSTECH, Dk. Amos Nungu wakizungumza na wanahabari.
   
Mkuu wa DFID, Natalie Smith akizungumzia wiki ya Ubunifu. Kushoto ni Mkurugenzi wa COSTECH, Dk. Amos Nungu na kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa HDIF, Joseph Manirakiza.
 Mkurugenzi wa Mawasiliano Vodacom, Rosalynn Mworia akizungumzia ushiriki wa Vodacom kwenye wiki ya Ubunifu. Kushoto ni Mwakilishi wa UNDP, Sergio Valdini.

NA IRENE MARK

MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk. Amos Nungu amesema serikali kwa kushirikiana na Mfuko wa Ubunifu Maendeleo ya Watu (HDIF), wamefanikiwa kiwezesha ajira 1,400 za kibunifu kwenye sekta mbalimbali.

Dk. Nungu alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akitangaza kuanza kwa wiki ya ubunifu inayofadhiliwa na Serikali ya Uingereza kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Kimataifa wa Uingereza (DFID) ambapo wabunifu zaidi ya 6,000 kutoka mikoa mbalimbali watashiriki.

Alisema maonesho hayo yatazinduliwa Machi 8 jijini Dar es Salaam NA Naibu Waziri wa Elimu, William ole Nasha yakibeba ujumbe usemao 'Buni kwa Tija' kisha kufanyika kwenye mikoa mingine Tanzania na Zanzibar.

Mkurugenzi mkuu huyo aliitaja mikoa itakayofikiwa na wiki ya ubunifu kuwa ni Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Mbeya, Arusha na Zanzibar huku akitarajia kuona bunifu zenye ufumbuzi wa changamoto za jamii.

"Bunifu ni eneo muhimu kwa maendeleo ya wananchi na jamii ndio maana COSTECH ilianzisha Buni Hub eneo linalokutanisha vijana wabunifu na kufanya shughuli zao hapo huku wakipata usimamizi kutoka kwetu," alisema Dk. Nungu.

Mkurugenzi Mkazi wa HDIF, Joseph Manirakiza alisema tangu mwaka 2015 walianza kufanya wiki ya ubunifu kwa kuzingatia sekta ya maji, afya, elimu na usafi wa mazingira ambapo bunifu mbalimbali zimefanikiwa kuondoa kero kwa wananchi.

"Baada ya wiki ya ubunifu tunachokifanya ni kuhakikisha wabunifu wanapeleka kazi zao kwa wadau wa maendeleo na serikali ili wapate fedha kwa ajili ya kuzifanyiakazi zaidi kwa maendeleo ya wananchi na jamii.

"Mfano sekta ya maji kwenye mji wa Maganzo wilayani Kishapu kule Shinyanga palikuwa hapana maji kabisa lakini chini kuna bomba kubwa la maji linatoa Maji ziwa Viktoria kupeleka Shinyanga.

"...  Ubunifu ukafanyika ikapatikana 'water atm' mwananchi unalipa kiasi kidogo cha fedha unapata maji, bunifu ile iliendelezwa sasa hivi ule mji wa biashara maji yapo kila mahali. Kwa hiyo yapo manufaa kwenye wiki ya ubunifu," alisema Manirakiza.

Kaimu Kiongozi wa DFID, Natalie Smith alisema ni mwaka wa sita sasa wanafadhili wiki ya ubunifu inayoonesha kukua na kufanikiwa hasa kutokana na ongezeko la washiriki na wadhamini wa wiki hiyo.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kampuni ya Vodacom, Rosalynn Mworia alisema ni mwaka wa pili kudhamini na kushiriki wiki ya ubunifu yenye mafanikio hasa kwenye utoaji wa huduma zao kwa jamii.

"Bunifu hizi tunazitumia kusaidia wakulima, wajasiriamali na wanafunzi kama ile ya shule softy ni matokeo ya bunifu za Vijana wa kitanzania hivyo nawakaribisha wananchi wote kushiriki kwenye wiki hii katika mikoa yao," alisema Mworia.

Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Sergio Valdini alisema wataendelea kuifadhili wiki ya ubunifu kwa kuwa ubunifu ni kiini cha biashara bora na kwamba wataendeleza prigramu za maendeleo kuelekea ajenda ya maendeleo ya mwaka 2030.

No comments:

Post a Comment

Pages