Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na Wakurugenzi pamoja na Watendaji wa
sekta ya ardhi katika mkoa wa Kagera (Hawapo pichani) jana wakati wa ziara yake
ya kikazi kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi mkoani Kagera. Kulia ni
Katibu Tawala wilaya ya Bukoba Kadole Kilugala na wa pili kushoto ni Kamishna
Msaidizi wa Ardhi Makwasa Biswalo.
Na Munir Shemweta, WANMM KAGERA
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Angeline Mabula ameonesha kutoridhishwa na
kiasi cha fedha kilichotengwa na halmashauri nane za mkoa wa Kagera kwa ajili
ya shughuli za kupanga, kupima na kumilikisha ardhi katika maeneo ya
halmashauri hizo.
Hali hiyo inafuatia
Naibu Waziri Mabula kuwahoji wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Kagera kutaka
kujua kila halmashauri ya mkoa huo imetenga kiasi gani cha fedha kwa ajili ya
shughuli za upangaji, upimaji na umilikishaji ardhi katika bajeti ijayo ya
mwaka 2020/2021 ikiwa ni juhudi za kuhakikisha maeneo yote yanapimwa ili
kuondoa migogoro ya ardhi na kuongeza mapato kupitia sekta ya rdhi.
Akiwa katika ziara yake
ya kikazi ya siku mbili mkoani Kagera jana Dkt Mabula alibaini halmashauri
mbili za Misenyi na Kyerwa katika mkoa wa Kagera ndizo angalau zilizoonekana kutenga
shilingi milioni 30 kwa kila moja kwa ajili ya shughuli za upangaji na upimaji
ardhi katika maeneo yao.
Kwa mujibu wa
mkurugenzi wa halmashauri ya Misenyi Innecent Mkandara halmashauri yake imetenga milioni
50 kwa ajili ya shughuli za ardhi na
milioni 30 kati ya hizo zitatumika kwa kazi ya upimaji huku mkurugenzi wa
Kyerwa Shadrack Magamba akieleza halmashauri yake kutenga milioni 30 kwa kazi
za upimaji sambamba na milioni 25 kwa ajili ya upimaji vijiji.
Halmashauri nyingine za
mkoa huo zimetenga chini ya milioni 30 huku halmashauri ya Karagwe ikiwa ya
mwisho kwa kutenga milioni 13 huku Mkurugenzi wake Godwin Kitonga akieleza kuwa
sehemu kubwa ya halmashauri inayofanyika shughuli ya urasimishaji.
Dkt Mabula alisema
kiasi kilichotengwa na halmashauri za mkoa wa Kagera katika kazi ya upangaji,
upimaji na umilikishaji ardhi ni kidogo sana na hakioneshi kama wakurugenzi wake
wana nia ya dhati ya kupima maeneo yao kwa kasi inayotarajiwa na wizara wakati
halmashauri hizo ndizo zenye mamlaka ya upangaji kwenye maeneo yake.
Hata hivyo, Naibu
Waziri wa Ardhi alisema katika kuhakikisha maeneo yote yanapangwa na kupimwa tayari
wizara imeanzisha utaratibu wa kuzikopesha halmashauri fedha isiyo na riba kwa
ajili ya shughuli za kupanga, kupima na kumilikisha maeneo ambapo kwa mwaka huu
wa fedha unaoisha halmashauri 24 zilikopeshwa
na nne kati ya hizo ndizo zilizofanikiwa kurejesha mkopo huo kwa asilimia mia
moja.
‘’Katika kipindi cha
mwaka wa fedha 2020/2021 Wizara ya Ardhi inatarajia kupatiwa bilioni saba kwa
ajili ya kuzikopesha halmashauri, ni vizuri wakurugenzi mkatumia fursa hiyo kwa
kuandika andiko litakalowawezesha kupata mkopo huo kulingana na maombi’’
alisema Dkt Mabula.
Sambamba hilo,
aliwataka wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Kagera kuhakikisha maeneo yote
ya umma yanapimwa kufikia mwezi julai mwaka huu na kupatiwa hati ili kuondoa
changamoto ya kuvamiwa na kupunguza migogoro ya ardhi ianyosababishwa na mipaka.
Akigeukia suala la mapato
yatokanayo ya kodi ya pango la ardhi, Dkt Mabula alisema mkoa wa Kagera unaweza
kuwa mkoa wa mwisho na kufuatiwa na ule wa Rukwa kwa kukusanya mapato kidogo ya
sekta ya ardhi. Hali hiyo inafuatia kuelezwa kuwa hadi sasa mkoa huo umekusanya
shilingi milioni 801 kati ya bilioni 3.3 ilizotakiwa kukusanya ambazo ni sawa
na asilimia 23.
‘’Kwa mtindo huu
hatuwezi kufika, tukisimamia vizuri sekta hii kwa kukusanya kodi ya ardhi
tutamsaidia mhe rais kusimamia miradi ya kimkakati ambayo mingi inaendeshwa kwa
fedha za ndani na sekta ya ardhi ikisimamiwa vizuri inaweza kukusanya fedha
kuliko sekta nyingine’’ alisema Mabula.
No comments:
Post a Comment