Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es
Salaam - Badru Idd (kushoto), akimkabidhi msaada wa madawati,
viti na meza 150 Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Kisare Makori (kulia) katika
Shule ya Sekondari Kibamba. Vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi milioni 15
vimetolewa na NMB kuzisaidia Shule tatu za Manispaa ya Ubungo ambazo ni Kibamba,
Kinzudi Sekondari pamoja na Shule ya Msingi Makuburi Jeshini zote za jijini Dar
es Salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Kisare
Makori (kulia mwenye suti), pamoja na Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es
Salaam- Badru Idd (wa pili kushoto) wakikata utepe kuzinduwa
madawati, viti na meza 150 katika Shule ya Sekondari Kibamba, vilivyotolewa na
Benki ya NMB kuzisaidia Shule tatu za Manispaa ya Ubungo ambazo ni Kibamba na
Kinzudi Sekondari na Shule ya Msingi Makuburi Jeshini kutatua changamoto za
madawati leo katika Manispaa ya Ubungo.
Na Mwandishi Wetu
BENKI
ya NMB, imekabidhi msaada wa viti, meza na madawati vyote vikiwa na
thamani ya Sh. Milioni 15 kwa ajili ya Shule za Sekondari Kibamba na
Kinzudi na Shule ya Msingi Makuburi Jeshini, zilizoko wilayani Ubungo
jijini Dar es Salaam.
Hafla
ya kukabidhi msaada huo ilifanyika katika viwanja vya Shule ya
Sekondari Kibamba, ambako Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Badru
Idd alimkabidhi msaada huo Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori
(aliyekuwa mgeni rasmi).
Alisema
Kibamba Sekondari yenye wanafunzi 1,365, ilikuwa na changamoto ya uhaba
wa viti na meza na kwamba msaada wa NMB unaenda kupunguza kwa kiasi
kikubwa adha ya wanafunzi kusoma katika mazingira yasiyo rafiki.
Naye
Ofisa Elimu (Sekondari) Wilaya ya Ubungo, Hilda Shalanda, alisema
kinachofanywa na benki ya NMB katika wilaya yake kwenye sekta ya elimu,
ni kitu cha kupongezwa na kinachopaswa kuungwa mkono na wadau wengine
kwa kuzifikia shule mbalimbali zenye uhitaji.
Aliongeza
kuwa, kwa niaba ya Halmashauri ya Ubungo, wanaishukuru NMB kwa kuwa
kimbilio la mahitaji ya kielimu wilayani mwake, huku akiwataka walimu na
wanafunzi wa shule zilizopokea vifaa hivyo, kuvitumia kwa ustaarabu na
kuvitunza.
#NMBKaribuYako
Akizungumzia
mgawanyo wa misaada hiyo, Badru alisema Shule ya Sekondari Kibamba na
Kinzudi kwa pamoja zimepewa viti 100 na meza 100 (sawa na viti 50 na
meza 50 kwa kila moja), huku Shule ya Msingi Makuburi Jeshini, ikipewa
madawati 100.
Alibainisha
kuwa, benki yake imekuwa na utaratibu wa kusaidia jamii kupitia
Programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), ambayo imetumika kwa karibu
miaka 10 sasa, ikitoa usaidizi wa utatuzi wa changamoto katika sekta za
elimu, afya na majanga.
“Ni
utamaduni tulioufanya kwa karibu miaka 10 sasa, lengo likiwa ni
kurejesha kwa jamii sehemu ya faida yetu ya kila mwaka, lakini pia
utaratibu huu unalenga kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha
sekta hizo na kuleta matokeo chanya,” alisema Badru.
Aliwataka
wanafunzi wa shule za Kibamba, Kinzudi na Makuburi Jeshini, kutunza
vifaa hivyo, ili viweze kutumika kwa muda mrefu na kusaidia wanafunzi wa
shule hizo watakaotumia kuepukana na adha za kusoma wakiwa sakafuni.
Akitoa
neno la shukrani baada ya kupokea vifaa hivyo, DC Makori aliishukuru
NMB kwa namna inavyoshikamana sekta za elimu na afya wilayani mwake na
kwamba kwa niaba ya Serikali, wanatambua na kuthamini mchango wa benki
hiyo.
“Kwa
hakika NMB ni wadau muhimu wa sekta ya elimu na afya wilayani Ubungo,
mmetusaidia mara kadhaa na tunawaomba msituchoke, tena muendelee kufanya
hivyo kila tutakapowakimbilia, ili kusaidia pale Serikali inapoishia
katika shule, zahanati na vituo vya afya,” alisema Makori.
Aliwataka
wadau zaidi wa elimu kujitosa kusaidia utatuzi wa changamoto za sekta
hiyo wilayani mwake kama inavyofanya NMB, na kubainisha kuwa wilaya yake
kwa sasa ina uhaba wa vyumba vya madarasa 100, pamoja na madawati 7,000
ili kutosheleza idadi ya wanafunzi waliopo.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Sekondari ya Kibamba, Natujwa Mrinde, kwa niaba ya
wakuu wa shule zilizosaidiwa, aliishukuru NMB na kuiahidi kuvitunza
vifaa hivyo, alivyokiri vimekuja kwa wakati muafaka, akiamini
vitachangia kukuza ufaulu katika shule hizo.
No comments:
Post a Comment