HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 20, 2020

TANESCO YATOA ZAWADI KWA MKAZI WA BIHARAMULO

Afisa Masoko wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Musa Chowo (kushoto), akikabidhi Sh. 500,000 kwa Dastan Paul aliyefanikisha kukamatwa wezi walioiba transfoma ya kilovoti 50, yenye thamani ya Sh. Milioni 6.



Na Alodia Dominick, Biharamulo

SHIRIKA la umeme Tanzania TANESCO limetoa kiasi cha 500,000 kwa Mwenyekiti  wa Kitongoji Chenkobe Kata ya Nyarubungo wilayani Biharamulo mkoani Kagera kama motisha ya kufanikisha kukamatwa wezi walioiba mashine umba (transfoma).

Afisa Masoko wa Shirika la Umeme (TANESCO), Musa Chowo, amekabidhi kiasi hicho cha fedha kwa Dastan Paul katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo.

Dastan Paul baada ya kukabidhiwa fedha hiyo, amesema kuwa, tukio la wizi wa transfoma lilitokea machi 5 mwaka huu majira ya saa 8 mchana wakati wezi wakiwa juu ya nguzo ya umeme alifika mwenyekiti huyo na kuwahoji ndipo walimwambia kuwa wametumwa na meneja wa Tanesco ili wakarekebishe kifaa kilichoharibika kwenye transfoma hiyo.

Ameeleza, baada ya kuwa na wasiwasi nao ndipo alitaka ampigie simu mwenyekiti wa kijiji hicho ambapo watu  hao wanaodhaniwa kuwa wezi walimwambia kama haamini waende naye hadi ofisi za Tanesco Biharamlo, ndipo alipanda gari hilo walipokaribia ofisi za tanesco aliona wamepita na kuelekea barabara ya Mwanza ambapo walimwambia wao wanaenda Buseresere hivyo wampe milioni 1.5 ili awaache waende.

Paul ameendelea kusimulia, wakiwa wanaendelea na safari alishika usukani ili gari lisimame huku dreva akiendelea kuendesha, gari lilianza kuyumba na ghafra aliona maaskari wa Jeshi la Wananchi Tanzania wakiwa katika kisima chao cha maji alianza kupiga kelele ndipo walisimamisha gari na wote waliokuwemo kwenye gari walishuka ambapo kati ya wanne waliokuwa kwenye gari hilo wanaodhaniwa kuwa wezi watatu walikimbia na kubaki mmoja.

Baada ya mahojiano na mmoja aliyebaki pamoja na mwenyekiti walijihakikisha kuwa transfoma imeibwa mwanajeshi mmoja alipiga simu polisi ndipo walifika na kumchukua kituo cha polisi Biharamlo dreva na mmoja kati yao ambaye alirudi baada ya kupigiwa simu huku wengine wawili walikuwa wameishazima simu zao.

Meneja wa shirika la umeme Tanzania Tanesco wilaya ya Biharamlo Ernest Milyango amesema kwamba, mradi ambao Mashine umba (transfoma) imeibwa unatekelezwa na Shirika hilo katika vijiji viwili vya Rusabura na Kabukoma katika vitongoji vinne, gharama zake mpaka  mradi ukamilike zitatumika shilingi milioni 857 ambapo ulianza decemba 20 mwaka jana na kwa sasa uko hatua za mwisho mafundi wakiendelea kufunga nyaya za njia ndogo na tayari transfoma tano zimeishafungwa katika njia kubwa.

Hata hivyo, katika mkutano huo meneja afya na usalama kazini wa TANESCO, Fred Kayega, akitoa elimu kwa wananchi juu ya kuweka tahadhari watakapoanza kutumia umeme amewataka wananchi kuwa walinzi wa miundo mbinu ya umeme na pale watakapobaini wezi watoe taarifa haraka katika uongozi wa kitongoji, kijiji, kata na wilaya ili wezi hao waweze kuthibitiwa.

No comments:

Post a Comment

Pages