Mkurugenzi
wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy
Matamwe akisisitiza umuhimu wa kutumia Dhana ya Afya moja ambayo
hujikita katika kujumuisha sekta zote za Afya katika kujiandaa,
kufuatilia na kukabili magonjwa yanayomuathiri binadamu wakati wa
mafunzo kwa timu za dharura za kukabili magonjwa ambukizi ya mlipuko
leo, Jijini Dodoma, tarehe 17 Machi, 2020.
Baadhi
ya wataalamu wa sekta za Afya kutoka kwa timu za dharura za kukabili
magonjwa ya mlipuko kutoka ngazi ya mkoa na wilaya zilizo mipakani,
wakifuatilia mafunzo ya kukabili magonjwa ya ambukizi ya mlipuko kwa
kutumia Dhana ya Afya moja, wakati wa mafunzo hayo, leo Jijini Dodoma,
tarehe 17 Machi, 2020.
Mkurugenzi
wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy
Matamwe akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu wa sekta za Afya
kutoka kwa timu za dharura za kukabili magonjwa ambukizi ya mlipuko
kutoka ngazi ya mkoa na wilaya zilizo mipakani, kwa kutumia Dhana ya
Afya moja, wakati wa mafunzo hayo, leo Jijini Dodoma, tarehe 17 Machi,
2020.
Na Mwandishi Wetu
Dhana
ya Afya moja ambayo hujikita katika kujumuisha sekta zote za Afya
katika kujiandaa, kufuatilia na kukabili magonjwa yanayomuathiri
binadamu imeendelea kufundishwa kwa Wataalamu wa sekta hizo za Afya,
ikiwa ni Sekta ya Afya ya Binadamu, Wanyamapori, Mifugo, Kilimo na
Mazingira, ili wataalamu hao watumie dhana hiyo kuimarisha udhibiti wa
magonjwa ambukizi kati ya Binadamu na wanyama ambayo hutokea mara kwa
mara katika maeneo ya mipakani kutokana na kuwepo kwa muingiliano
mkubwa kati ya watu na wanyama katika mazingira yao.
Katika
kuimarisha Afya ya binadamu, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa
Mataifa (FAO), pamoja na watalaamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Chuo
Kikuu cha Kilimo Sokoine wamewapa mafunzo wataalamu wa sekta za Afya
wanao toka katika Halmashauri za Mkoa wa Kagera, Rukwa, Katavi, Rukwa
na Songwe zilizo mipakani juu ya namna ya kujiandaa na kukabili magonjwa
ambukizi ya mlipuko kama vile Ugonjwa wa Corona na Ebola kwa kutumia
Dhana ya Afya moja.
Akiongea
wakati wa kufungua mafunzo hayo leo tarehe 17 Machi, 2020, Jijini
Dodoma, Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri
Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe, amebainisha kuwa ushirikiano wa wataalam na
sekta za Afya kwa kutumia dhana ya Afya Moja hivi sasa ni agenda ya
dunia nzima. Aidha, ameeleza kuwa Dhana hiyo imekusudiwa kutumika maeneo
ya mipakani ambapo mwingiliano huo huchochewa na wasafiri kutoka eneo
moja kwenda jingine, ongezeko la watu duniani, mabadiliko ya tabia
nchi, utandawazi, ongezeko la mahitaji ya maji na chakula.
“Mafunzo haya ni muhimu sana nchini kwa kujenga uwezo wa nchi katika utayari wa kukabiliana na magonjwa yanayosambazwa na wanyama na kuathiri wanyama na binadamu.Tanzania tumeabiwa yupo mgonjwa wa Corona19, ambapo Tumeambiwa
mgonjwa anaendelea vizuri na matibabu, na serikali inaendelea kuchukua
hatua za madhubuti za kuhakikisha ugonjwa huu unadhibitiwa ili usisambae
nchini”.
Awali
akiongea katika mafunzo hayo, Mkuu wa Ndaki ya Mifugo, Chuo Kikuu cha
Kilimo cha Sokoine-SUA, Profesa, Amandus Muhairwa amebainisha kuwa
sekta za Afya zikishirikiana katika Kudhibiti magojwa zitasaidia
kuimarisha Afya ya Binadamu kwa kuwa kila sekta itakuwa inachukuwa
tahadhari kwa wakati.
Aidha,
Mratibu kutoka FAO wa Mradi wa ECTAD Tanzania, Fasina Folorunso
amabainisha kuwa FAO inaendelea kushirikiana na serikali mya Tanzania
kupitia Dawati la Afya moja katika kujenga uwezo wa kukabiliana na
magonjwa ambukizi ya mlipuko kwenye ngazi ya mkoa na wilaya hususani
maeneo ya mipakani.
Katika
kuhakikisha watalaam hao kutoka sekta za Afya wanaweza kutumia Dhana
hiyo katika kudhibiti magonjwa katika maeneo ya mipakani wameweza
kujengewa uwezo wa namna ya kutoa taarifa za milipuko ya magonjwa
ambukizi kama vile ugonjwa wa Corona 19 na Ebola yanapotokea maeneo ya
mipakani, namna ya kuunda vikosi vya kufuatilia na kukabili Ugonjwa,
Mawasiliano wakati wa kufuatilia na kukabili magonjwa hayo kwa kutumia
Dhana ya Afya moja, pamoja na masuala ya kutumia vifaa Kinga Binafsi
vya Kitaalamu.
Tarehe
13 Februari 2018, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Kassim Majaliwa alizindua Dawati la Uratibu la Afya moja chini ya Ofisi
ya Waziri Mkuu, likiwa na lengo la kusimamia na kuratibu shughuli za
Afya moja nchini. Kwa kutambua umuhimu huo Idara ya Uratibu Maafa Ofisi
ya Waziri Mkuu, kupitia Dawati la Uratibu wa Afya moja kwa kushirikiana
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) wakishirikiana
na USAID, OIE, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine - SUA wakishirikiana
na Chuo Kikuu cha Kansas cha nchini Marekani waliandaa na kuratibu mafuzo hayo.
No comments:
Post a Comment