Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa
Kamati Maalum aliyoiunda ya kuchunguza zao la mkonge, Gerlad Kusaya
baada ya taarifa hiyo kusomwa mbele ya Waziri Mkuu katika kikao kati
ya Waziri Mkuu na watumishi na viongozi wa Halmashauri za Mkoa waTanga
kilichofanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Naivera jijini Tanga, Machi
1, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Na Mwandishi Wetu, Tanga
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea taarifa ya uchunguzi wa tuhuma mbalimbali katika tasnia ya kilimo cha mkonge mkoani Tangana kuagiza mapendekezo yaliyotolewa na timu hiyo yakiwemo ya kurejeshwa Serikalini kwa nyumba na. 176 eneo la Bombo ambayo ilimilikishwa kwa Bw. Salum Shamte yafanyiwe kazi.
Nyumba
nyingine zilizopendekezwa kurejeshwa Serikalini ni pamoja na nyumba
kumi zilizoko ndani ya Jiji la Tanga katika maeneo ya Raskazone, Bombo,
Nguvumali na Market street ambazo zilinunuliwa na watumishi hao kwa
udanganyifu.
Waziri
Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumapili, Machi 1, 2020) wakati
akizungumza na watumishi wa halmashauri za mkoa wa Tanga, viongozi wa
taasisi mbalimbali, wadau wa zao la mkonge pamoja na viongozi wa dini
kwenye ukumbi wa hoteli ya Naivera.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wawekezaji ambao wanamiliki mashamba
ya mkonge yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 2,000 ambao hawajayaendeleza
wayaendeleze wakishindwa yatachukuliwa na kugawiwa kwa wananchi.
Timu
hiyo maalum ya uchunguzi iliundwa na Waziri Mkuu na ilifanya uchunguzi
mkoani Tanga kuanzia tarehe 29/11/2019 hadi tarehe 07/02/2020. Timu hiyo
iliyokuwa na wajumbe 13 ilihusisha maafisa kutoka ofisi mbalimbali za
Serikali.
Uchunguzi
huo maalum ulihusu masuala mbalimbali katika tasnia ya zao la mkonge
mkoani Tanga ambayo ni pamoja na uzalishaji wa mkonge, bei ya zao la
mkonge katika soko la ndani na nje ya nchi.
Pia,
ilichunguza kuhusu mali za iliyokuwa Mamlaka ya mkonge nchini, ubia
kati ya Kampuni ya Katani Limited na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii
(NSSF), Utendaji kazi wa Kampuni ya Katani Ltd na pia Utendaji kazi wa
Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB).
Awali,Mwenyekiti
wa timu hiyo Bw. Gerald Kusaya alisema timu ilibaini kuwa Kampuni ya
Katani Ltd tokea mwanzo ilikuwa na mgongano wa kimaslahi na kupelekea
kuhujumu uchumi kwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wake Bw. Salum Shamte
alikuwa mtumishi wa umma na alishiriki vikao vyote vya ubinafsishaji wa
Mamlaka ya Mkonge ilhali akijua kuwa ana maslahi kwenye Kampuni
inayonunua.
“Kwa
kuwa uchunguzi umebaini viongozi na wanahisa wa Katani Ltd waliohusika
kuingia mikataba walikuwa watumishi wa Mamlaka ya Mkonge wakati wa
mchakato wote wa ubinafsishaji hivyo walitumia vibaya madaraka yao kwa
kuishawishi Serikali kuingia mkataba huo usiokuwa na tija kwa Serikali
bali kwa manufaa yao binafsi. Hivyo, Timu imeandaa taratibu kwa ajili ya
wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.”
Bw. Kusaya amesema timu hiyo inapendekeza kuwa Serikali
itoe fedha kwa ajili ya kazi ya kuyapima upya mashamba matano ya
Mwelya, Ngombezi, Hale, Magunga na Magoma ili wananchi wanaoendelea
kutumia mashamba hayo kwa kukodishwa na Bodi ya Mkonge kama
ilivyokubalika kwenye Baraza la Mawaziri mwaka 2005 ili waweze kupewa
Hati ndogo (leasehold tittle);
Alisema
timu inapendekeza nyumba 30 zilizopo eneo la Muheza, ambazo baadhi
zilitolewa kwa wananchi waliokuwa watumishi wa Mamlaka ya Mkonge na
baadhi kuachwa kwa ajili ya makazi ziendelee kuwa mali ya wananchi hao
kwa kuwa eneo hilo kwa sasa lipo chini ya Halmashauri ya Wilaya ya
Muheza.
“Nyumba
22 zilizoko ndani ya mashamba ya mkonge na maeneo ya kiwanda cha
TANCORD ziendelee kubaki mali ya Serikali na nyumba iliyoko katika
kiwanja Na. 176 eneo la Bombo iliyohamishwa kwenda kwa Ndg. Salum Shamte
irejeshwe Serikalini kwa njia ya urekebishaji wa daftari la Msajili wa
Hati.”
Kwa upande wao,
viongozi wa mkoa wa Tanga wakiwemo wabunge wamemshukuru Waziri Mkuu kwa
kuunda timu hiyo ya uchunguzi wa zao la mkonge kwa kuwa mapendekezo
yake yamejibu changamoto zilizokuwa zinalikabili zao hilo.
Wamesema
mapendekezo yaliyotolewa na timu hiyo yanakwenda kufufua kilimo cha zao
la mkonge hivyo kuongeza tija kwa wakulima wa mkonge mkoani Tanga.
No comments:
Post a Comment