Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua bwalo la chakula na madarasa, katika Shule ya Sekondari ya bweni ya Lucas Malia, iliyopo wilayani Ruangwa, mkoani Lindi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka wanafunzi wanaosoma katika shule ya
Sekondari ya Wasichana ya Lucas Malia wilayani Ruangwa wasome kwa bidii
kwa sababu Serikali imewaboreshea mazingira na kuwaepusha na vishawishi.
“Mawazo
na akili yenu yote iwe katika kusoma tu, tunataka kuona mkiendelea
kusoma hadi kidato cha tano na sita ili ndoto zenu za kufika vyuo vikuu
zitimie.”
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Machi 16, 2020) wakati akizungumza
na walimu na wanafunzi alipotembelea na kukagua maendeleo ya shule hiyo
ya wasichana iliyopo wilaya ya Ruangwa, Lindi.
Shule
ya Sekondari ya Wasichana ya Lucas Malia ni ya bweni na ilibadilishwa
kutoka shule ya msingi Mnacho ambayo ilianzishwa mwaka 1932 na Shirika
la Wamisionari Wakatoliki chini ya Mwalimu Lucas Malia.
Waziri
Mkuu ambaye alisoma katika shule msingi Mnacho kabla ya kubadilishwa,
amesema mwaka 2017 alitembelea shule hiyo na kukuta majengo yamechakaa
ndipo alipotafuta wadau na kuyafanyia ukarabati.
“Nilikuta
hata jengo ambalo nilisomea lilikuwa limechakaa, tulitafuta fedha na
kukarabati ikawa mpya. Tuliamua kufanya mabadiliko kwa kuzingatia watoto
waliokuwa wakisoma hapa walikuwa wanatoka kijiji cha Ng’au na kipindi
cha mvua walishindwa kuja shule kutokana na mto kujaa maji.”
Waziri
Mkuu ameongeza kuwa baada ya kubadilisha shule hiyo na kuwa ya
sekondari ya wasichana walijenga shule ya msingi katika kijiji cha Ng’au
na kuwahamishia watoto waliokuwa wakisoma shule ya msingi Mnacho.
Amesema
katika wilaya ya Ruangwa hakukuwa na shule ya sekondari ya wasichana,
hivyo amefarijika sana kuona watoto wa kike wakianza kusoma kidato cha
kwanza kwenye shule hiyo ya bweni.
Waziri
Mkuu amesema lengo ni kuhakikisha shule hiyo inakuwa na kidato cha tano
na sita kwa sababu ina vyumba vya madarasa na mabweni ya kutosha.
“Kuwepo kwa kidato cha tano na sita kutawaongezea ari ya kusoma
wanafunzi wengine.”
Kwa
upande wao, wanafunzi wanaosoma kwenye shule ya Sekondari ya Wasichana
ya Lucas Malia wameishukuru Serikali kwa kuanzisha shule hiyo kwakuwa
imewaepusha na vishawishi.
Wakiongea
kwa niaba ya wanafunzi wenzao, Sharifa Mbunga, Irene Mkuti, Ikra Jirani
na Mwanayazi Omary wamesema uwepo wa shule hiyo utaongeza ari ya kusoma
kwa wanafunzi wa kike wilayani Ruangwa, hivyo wameahidi kusoma kwa
bidii.
Kwa upande wake,
Kaimu Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Gladness Makongwa amesema shule
imedahili wanafunzi 75 wa kike waliopata ufaulu wa juu kutoka kata zote
zilizo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa.
No comments:
Post a Comment