Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo.
Na Mwandishi Wetu
Katika harakati za
kupambana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona
(COVID – 19) Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametoa maelekezo kwa wananchi
wa mkoa wa Rukwa kuhakikisha wanavaa barakoa wanapokuwa katika mikusanyiko pamoja
na maeneo yao ya kibiashara hasa kwa wale wanaohusika na kutoa huduma kwa jamii
huku akivitaka vyombo husika kuhakikisha abiria wote wanaotoka katika maeneo yaliyoathirika
ndani ya nchi kuingia mkoa wa Rukwa washauriwe kujitenga kwa hiari kwa muda wa
siku 14.
Mh. Wangabo amesema
kuwa abiria hao wanaoingia ndani ya mkoa wanatakiwa kupimwa afya zao kwa kipima
joto (Thermal Scanner) kwenye vituo vitatu vya mabasi mkoani humo ikiwemo Laela
kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Kituo cha mabasi Namanyere
kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi pamoja na kituo kikuu cha mabasi
Sumbawanga na kuongeza kuwa abiria hao wanatakiwa kuvaa Barakoa.
“Abiria wanaoingia
Mkoa wa Rukwa kutoka kwenye maeneo yaliyoathirika wanashauriwa kujitenga wao
wenyewe kwa hiari yao kwa muda wa siku kumi na nne (14). Endapo watahisi au
kugundua kuwa wanaona dalili zozote za matatizoya kiafya watatakiwa kuripoti
kwenye kituo chochote cha Afya cha karibu,” Alisema.
Aidha, Mh. Wangabo
amewashauri wafanyabiashara wote ndani ya mkoa wenye tabia za kusafiri kwa nia
ya kufuata mizigo ya kibiashara kuacha kufanya hivyo na badala yake wajenge
tabia ya kuagiza bidhaa hizo kwa njia ya sim una kulipa kwa njia za mitandao ya
simu ama benki inapobidi na pia kuwashauri wafanyabiashara wadogo kujiunga na
kuagiza mzigo kwa pamoja ili kuwa na urahisi wa kupata usafiri wa pamoja.
“Watu wote wanaofanya
kazi za kutoa huduma kwenye maduka, Maeneo yote ya kuuza vyakula, Saluni, Super
Market, Wahudumu wa nyumba za kulala Wageni wanatakiwa kuvaa barakoa. Familia zinapotaka
kufanya manunuzi ya jumla, inashauriwa aende mtu mmoja tu kutoka kila familia
kufanya manunuzi hayo. Hata kwenda hospitali kuona wagonjwa aende mtu mmoja tu
na mtu huyo asisahau kuvaa barakoa,” Alisisitiza.
Halikadhalika,
amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha kuwa minada yote na Magulio
inadhibitiwa na kuendeshwa kulingana na maelekezo ya wataalamu wa afya na
serikali kwa ujumla, na kubainisha kuwa serikali ya mkoa haitasita kusitisha
mnada ama gulio endapo taratibu na maelekezo ya wataalamu ama ya serikali
yatakiukwa.
Mh. Wangabo ameyasema
hayo katika taarifa yake aliyoitoa leo tarehe 20.4.2020 kwa vyombo vya habari.
Kwa mujibu wa taarifa
kutoka kwa Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy
Mwalimu hadi kufikia tarehe 20.4.2020 watu waliopata maambukizi ya ugonjwa wa
Corona nchini ni 257 ambapo kati ya hao mkoa wa Rukwa ina wagonjwa wawili (2).
No comments:
Post a Comment