Zoezi la upulizaji wa dawa kwenye mabasi katika Stendi kuu ya Nzega
Mkoani Tabora ukiendelea leo kama sehemu ya mkakati wa kukabiliana na
Virusi vya Corona.
Na Tiganya Vincent
MKUU wa Mkoa
wa Tabora Aggrey Mwanri amesimamisha kwa muda likizo za watumishi wakiwemo wa
Idara za Afya ili waendelee kuunganisha nguvu katika kusaidia jamii kwenye
kampeni za mapambano ya ugonjwa wa Covid -19.
Hatua hiyo
inalenga kuhakikisha kuwakuwepo na wataalamu wa kutosha katika maeneo yote
ambao wataendelea kutoa elimu ya kujikinga na kudhibiti ugonjwa wa homa kali ya
mapafu unaosababishwa na virusi aina ya Corona usiingie Mkoani Tabora.
Mwanri alitoa
kauli hiyo jana wilayani Uyui na Nzega wakati ziara yake ya kukagua Vituo na
Zahanati zilizoandaliwa kwa ajili ya washukiwa wa ugonjwa wa covid -19 kama
itatokea bahati wakaonekana wakaonekana Mkoani humo.
Alisema
kipaumbele hivi sasa ni kuhakikisha tahadhari zote zinachukuliwa ili wakazi wa
Mkoa wa Tabora waendelee kuwa salama kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu na
viongozi wa Kitaifa.
Aidha Mwanri
alizitaka Halmashauri zote za Mkoa wa Tabora kutumia redio zilizopo na magari
ya matangazo kupeleka elimu katika maeneo mbalimbali ya wananchi juu ya
kujikinga na kulinda dhidi ya Covid -19.
“Tumieni
magari yenye vipaza sauti kupitia katika mitaa mbalimbali kutoa elimu ya
kujikinga wakati wote…na pia wataalamu nendeni katika Redio zote zilizopo
mkoani Tabora kupeleka ujumbe ambao utawasaidia wananchi kuepuka kupata
maambukizi ya Corona” alisema.
Katika hatua
nyingine Mkuu wa Mkoa ameziagiza Halmashauri zote kuhakikisha magari yote ya
abiria yanayosafirisha abiria ndani na nje Mkoa wa Tabora yanapuliziwa dawa
kabla ya safari ili kuwakinga abiria ya uwezekano wa kupata corona.
Alisema ni
lazima gari linapofika Stendi lipuliziwe dawa na taarifa zake zijazwe kwenye
fomu ili kuonyesha kuwa limetekeleza agizo hilo ndio liruhusiwe kupakia abiria
na kuendelea na safari zake.
No comments:
Post a Comment