Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff akiwa kwenye
kikao kazi na Waratibu wa TARURA wa Mikoa, kwenye kikao kilichofanyika katika ukumbi
wa Mikutano wa TARURA Makao Makuu- Mtumba jijini Dodoma hivi karibuni.
Na Erick Mwanakulya
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff amewataka
Waratibu wote wa TARURA nchini kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika barabara
na madaraja ili kubaini maeneo yanayohitaji ukarabati na kuyafanyia kazi kabla
ya kuleta madhara.
Mhandisi Seff ameyasema
hayo, alipokutana na Waratibu wa TARURA wa Mikoa jijini Dodoma katika ukumbi wa
Mikutano wa Ofisi za TARURA Makao Makuu zilizopo Mtumba, ikiwa ni sehemu ya
kikao kazi kilicholenga kutoa maelekezo na miongozo mbalimbali ya ufanyaji kazi
ili kuwapatia wananchi huduma ya usafiri na usafirishaji.
Aidha, Mtendaji Mkuu amesisitiza
kuwa, ukaguzi wa mara kwa mara wa miundombinu unasaidia kupunguza gharama kwani
uharibifu au uchakavu wa miundombinu ukibainika mapema ukarabati wake unaweza
kufanyika katika hatua za awali kwa gharama nafuu na kwamba miundombinu
inapoharibika moja kwa moja gharama inakuwa kubwa sana pale inapobidi kujengwa
upya.
Pia, Mhandisi Seff
amesisitiza juu ya uwekwaji wa alama za barabarani hasa katika maeneo maalumu
kama madaraja na maeneo yaliyoharibika ili watumiaji wa barabara watambue
vizuri maeneo hayo wakati wa kupita.
‘‘Natoa
maelekezo juu ya uwekwaji wa alama za barabarani kwamba, hakikisheni mnaweka
alama za kudumu maana sitamsikiliza yeyote atakayekuja na sababu kuwa kibao
kimeibiwa wakati angeweza kuweka kibao cha kudumu hata kwa kutumia zege maana
bila kuwa na alama hizo inaweza kuwa chanzo cha ajali”, amesisitiza
Mhandisi Seff.
Ili kurahisisha usimamizi
wa kazi kwa mikoa yote kiongozi huyo ameeleza kuwa, anaendelea kutoa magari kwa
Waratibu wote wa TARURA na kisha atatoa magari kwa Mameneja wa TARURA wa
Halmashauri ili kuhakikisha wanasimamia kazi na wananchi wanasafiri kwa
urahisi.
Wakala wa Barabara za
Vijijini na Mijini (TARURA) unaendelea kutekeleza majukumu yake katika Mji wa
Serikali Mtumba baada ya kukamilisha ujenzi wa ofisi yake na kuhamia rasmi.
No comments:
Post a Comment