Na Mwandishi Wetu
Benki ya CRDB imezindua mpango maalum wa uwezeshaji sekta ya afya nchini katika Kongamano la Wadau wa Sekta ya Afya “Afya Forum”lililoandaliwa na Benki ya CRDB.
Akizungumza katika Kongamano hilo lillilofanyika kwa njia m tandao na kuhudhuriwa na watoa huduma za afya zaidi ya 500, Naibu Wazir i wa Afya, Dkt. Godwin Mollel ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuzindua mpango huo ambao utakwenda kusaidia kuondoa changamoto ya fedha za uendeshaji na uwekezaji katika miradi ya afya kwa hospitali, vituo vya afya na zahanati za umma na binafsi.
“Mpango wetu katika Serikali ni kuona tunaboresha ubora na upatikanaji wa huduma kwa Wananchi kupitia miradi na programu mbalimbali kwa kushirikiana na sekta binafsi ikiwamo taasisi za fedha. Ninafurahi kuona utayari wa Benki ya CRDB katika kushirikiana na Serikali kufanikisha azma hii ya kuhakikisha Watanzania wanapata huduma za afya zilizo bora zaidi,” alisema Dkt. Godwin Mollel.
Dkt. Godwin Mollel alisema mpango huo wa uwezeshaji sekta ya afya wa Benki ya CRDB umekuja katika kipindi muhimu ambapo taifa lipo katika mjadala wa uboreshwaji wa huduma za afya kutokana na changamoto iliyojitokeza ya mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu ujulikanao kitaalamu COVID19.
“Nidhahiri kuwa mahitaji ya huduma za afya kwa upande wa dawa, vifaa tiba na miundombinu yameongezeka kwa kiasi kikubwa kipindi hiki cha janga la corona. Niishukuru Benki ya CRDB kwa kuja na huduma na bidhaa mahsusi zitakazosaidia watoa huduma za afya kuendana na ongezeko hili la mahitaji lakini pia kutatua changamoto zilizokuwepo,” aliongezea Dkt. Godwin Mollel
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema kwa muda mrefu Benki hiyo imekuwa ikitoa mikopo ya kusaidia kuboresha sekta ya afya nchini, ambapo hadi sasa mikopo ya zaidi ya shilingi bilioni 78 imeshatolewa kwa zaidi ya hospitali100 nchini nzima.
Pamoja na jitihada hizo Nsekela amesema Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Serikali na wadau wengine wa sekta ya afya imekuwa ikiendelea kufanyia kazi changamoto zinazoikabili sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya nchi kwa kubuni huduma na bidhaa zitakazosaidia kutatua changamoto hizo ikiwamo uwekezaji katika viwanda vya vifaa tiba na dawa ili kupunguza gharama katika sekta hiyo.
“Tukiwa Benki ya kizalendo tunajukumu la kuhakikisha tunatoa masuluhisho ya kifedha na kimiundombinu ilikusaidia kubo resha utoaji wa huduma na ukusanyaji wa mapato katika hospitali na vituo vya afya,” alisema Nsekela huku akibainisha kuwa Benki hiyo tayari imeshafanikiwa kuunganisha mfumo wake wa malipo wa kidijitali kwa zaidi ya hospitali 144 nchi nzima ambao unawezesha wateja kufanya malipo kupitia njia za kidijitali kama TemboCard, SimBanking, Internet banking na mfumo wa malipo kupitia QR-Code.
Nsekela alisema katika mpango huo wa uwezeshaji sekta ya afya, Benki ya CRDB inatoa mikopo ya ununuzi wa mashine za kitabibu kwa ajili ya kusaidia upatikanaji wa matibabu ya kisasa na mikopo ya uendeshaji ili kusaidia hospitali katika gharama za ununuzi wa madawa na vifaa tiba.
“Watoa huduma wengi wa afya wamekuwa wakipata changamoto ya fedha za uendeshaji kutokana na ucheleweshwaji wa malipo ya gharama za matibabu. Kupitia huduma zetu za mikopo za overdraft na invoice discounting tumedhamiria kusaidia kuondokana na changamoto hii kwa kushirikiana na Bohari ya Taifa ya Dawa (MSD), Mfuko wa Taifa wa Bima, na watoa huduma wengine wa bima,” alisema Nsekela huku akibainisha Benki hiyo pia inatoa mikopo kwa wasambazaji wa vifaa tiba na dawa ambao wanahitaji fedha kwa ajili ya kukamilisha mkataba wa kazi (LPO financing).
Kwa upande wa miradi mikubwa ya afya, Nsekela alisema Benki ya CRDB imejipanga kushirikiana na washirika wake wa nje na ndani kusaidia upatikanaji wa fedha kukamilisha miradi hiyo.“Tukiwa Benki kubwa nchini tumejidhatiti kimtaji kuhakikisha tunafanya uwezeshaji unaotakiwa hii ikiwa ni pamoja na kushirikiana na washirika wetu,” aliongezea Nsekela.
Wadau wa sekta ya afya waliohudhuria Kongamano hilowameipongeza Benki ya CRDB kwa jitihada hizo za kuboresha sekta ya afya nchini huku wakibainisha kuwa itasiaidia kuongeza tija katika sekta ya afya kwa kuwezesha kutoa huduma bora za afya kwa Wananchi.
“Niwasishi watoa huduma za afya wote kuchangamkia fursa hii inayotolewa na Benki ya CRDB ilituweze kuboresha huduma zetu na kufanya uwekezaji wenye tija utakaokuwa na Maendeleo katika sekta ya afya na taifa letu kwa ujumla,” alisema Dkt. Samuel Ogilo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Watoa Huduma za Afya Binafsi (APHFTA)
Kongamano hilo la uwezeshaji sekta ya afya lililoandaliwa na Benki ya CRDB, lilihudhuriwa na viongozi na wakuu wa taasisi mbali ikiwamo Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania, Elisha Osati, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima, Bernard Konga na mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa, Victoria Elangwa, Mkurugenzi wa Taasisi ya Benjamin Mkapa,Dkt. Gabriel Mhidize, Ellen Mkondya.
No comments:
Post a Comment