HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 31, 2020

Kisarawe kusajili shule ya wasichana

Moja ya jengo jipya na la kisasa la Shule ya Sekondari ya Wasichana Jokate Girls iliyopo Kata ya Kibuta wilayani Kisarawe mkoani Pwani ambayo linavyoonekana.Waziri
wa Nchi ,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemen Jafo amefanya ziara ya kutembelea shule hiyo kwa ajili ya kukagua maendeleo ya ujenzi wake.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo (katikati
aliyevaa gauni) akiwa na wana kamati wa kujitolea ambao
wameshiriki kikamilifu katika ujenzi wa shule ya bweni ya
wasichana ambayo Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Rais Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Selemen Jafo
ameagiza iitwe Jokate Girls Sekondari.
 Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Jokate Mwegelo akizungumza mbele ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) kuhusu maendeleo ya ujenzi wa shule ya bweni ya wasichana inayojengwa Kijiji cha Mhaga ,Kata ya Kibuta wilayani humo.Majengo ya shule hiyo ni ya kisasa zaidi.
Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemen Jafo akizungumza
jana baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya
bweni ya wasichana inayojengwa Kijiji cha Mhaga katika
Kata ya Kibuta wilayani Kisarawe.Waziri Jafo ameagiza
shule hiyo ipewe jina la Jokate Girls Sekondari kama
sehemu ya kutambua na kuthamini mchango wa Mkuu wa
Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo ambaye ndiyo
ameijenga.


Na Mwandishi Wetu
 
 
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo amemuelekeza mkurugenzi wa Halmashauri ya Kisarawe na Ofisa Elimu wa wilaya hiyo kuanza  mchakato wa usajili jina la shule ya sekondari ya wasichama huku akitaka iitwe Jokate Girl School.

Waziri Jafo alisema hayo jana baada ya kukagua ujenzi wa shule hiyo ambapo amesema ameridhishwa na hatua ya ujenzi ilipofikia.

Alisema shule hiyo ya wasichana imejengwa katika kijiji ya Mhaga, kata ya Kibuta wilayani Kisarawe mkoani Pwani na itakuwa na mchango mkubwa kwa watoto wa kike wa Kisarawe, Pwani na nchi kwa ujumla.

"Natoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe na Ofisa Elimu Wilaya kuanza mchakato wa kusajili jina ila ingendeza ikiitwa Jokate Girls School kama sehemu ya kutambua mchango na jitihada za Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo ambaye amefanikisha kujengwa kwa shule hiyo ya kisasa wilayani humo," alisema.

"Shule hii kwasababu DC wangu ulibeba maono, shule hii nataka niite Jokate. Huo ndio uamuzi wangu na sababu kubwa DC Jokate aliamua ufanya kazi na kubeba maono yangu mimi, shule nzuri sana kama ulivyo mweyewe na Mungu akubariki sana.Tunataka shule hii iwe bora sana hapa nchini,"alisema Waziri Jafo huku akimwagia Sifa Jokate kwa kazi kubwa ambayo ameifanya na kwamba Jokate ni moja ya wakuu wa Wilaya bora nchini.

Akifafanua zaidi Waziri Jafo alisema nguvu kubwa ya utendaji wa Jokate katika shule hiyo ndio umemfanya kuamua iitwe jina lake na kwa Kisarawe kuna kila sababu ya kutambua moyo wa uzalendo na upendo wa mkuu huyo wa wiilaya kwa kumpa heshima hiyo.

"Narudia tena kueleza hapa hadharani DC Jokate anafanya kazi sana tena kwa vitendo , ni mbunifu na anabeba maono yenye uzalendo mkubwa kwa nchi yake.Katika Wilaya ya Kisarawe wamepita viongozi wengi sana lakini sijawahi kuona kiongozi mchapa kazi kama Jokate na kutoka moyoni namtakia heri katika utendaji wake na Mungu amsimamie apande zaidi ya hapa alipokuwa,"alisisitiza.

Waziri Jafo ametumia nafasi hiyo kuifichua siri ya uchapakazi wa Jokate ndani ya Wilaya ya Kisarawe  kwani baada ya Rais John Magufuli kumteua kwenye nafasi hiyo alimuita ofisini kwake na kisha kumueleza kuhusu Kisarawe na hakika ametenda haki kwani yote ambayo amemueleza ameyafanyia kazi kwa asilimia 100 na wananchi wa wilaya hiyo ni mashahidi.

"Wananchi wa Kisarawe naomba leo niwaambie baada ya kufanya mazungumzo na Jokate baada ya kuteuliwa na Rais, nilimueleza mambo mengi na leo hii amenithibitishia kwa vitendo niliyomueleza yalimuingia na ameyabeba maono yangu.

Kisarawe tumepata bahati kubwa ya kuwa na Jokate pamoja na viongozi wengine akiwemo Mkurugenzi na Katibu Tawala ambao wote ni vijana na wazalendo kwa nchi yetu,"alisema Waziri Jafo.

Kwa upande wake Jokate akizugumza baada ya Waziri Jafo kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule hiyo , alisema anawashukuru watu wote ambao wameshiriki kila hatua kuhakikisha ujenzi wa shule hiyo unafanyika na hana cha kuwalipa zaidi ya kuwaomba waendelee na moyo wa uzalendo na kuipenda nchi yao.

"Tumefika hapa leo na shule yetu inaonekana ilivyo kwasababu watu waliamua kubeba maono yetu ya Tokomeza Zero Kisarawe kwa moyo mmoja, wamejitoa kwa michango na mawazo, nawashukuru wote,"alisema Jokate na kusisitiza kuwa Kisarawe wao wataendelea kuchapa kazi kama ambavyo Rais Magufuli amekuwa akisisitiza siku zote.

No comments:

Post a Comment

Pages