Mkuu wa Wilaya ya Tarime Injinia Mtemi Msafiri
akiangalia baadhi ya mimea iliyopandwa kama Tegesha katika kijiji cha Komorera
eneo la Nyamongo wilaya ya Tarime mwishoni mwa wiki alipokwenda kutangaza
notisi ya kusitisha maendeleo katika eneo hilo kupisha shughuli za uchimbaji
madini katika mgodi wa Barrick North Mara. (Picha na Wizara ya Ardhi).
Mthamini Mkuu wa Serikali Evelyne Mugasha akizungumza wakati wa utoaji notisi
ya kusitisha maendelezo katika kijiji cha Komorea eneo la Nyamongo wilayani
Tarime mkoa wa Mara mwishoni mwa wiki
kupisha shughuli za uchimbaji madini katika mgodi wa Barrick North Mara.
Kushoto kwa Evelyne ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime Injinia Mtemi Msafiri na
kushoto ni Katibu Tawala wilaya John Marwa.
Sehemu ya wakazi wa kijiji cha Komorera kata ya Nyamongo wilaya ya Tarime mkoa
wa Mara wakimsikiliza Mthamini Mkuu wa Serikali (hayupo pichani) wakati wa
kutangazwa notisi ya kusitisha maendelezo katika eneo hilo mwishoni mwa wiki
kupisha shughuli za uchimbaji madini katika mgodi wa Barrick North Mara.
Na Munir Shemweta, WANMM TARIME
Serikali
imewatahadharisha wananchi wa kijiji cha Komarera kata ya Nayamongo Tarime
Vijijini mkoani Mara kuacha tabia ya kufanya maendelezo maarufu kama Tegesha
katika eneo linalotaka kuchukuliwa na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara
kwa shughuli za uchimbaji madini.
Tahadhari hiyo
imetolewa mwishoni mwa wiki Nyamongo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara na Mthamini
Mkuu wa Serikali Evelyne Mugasha wakati wa kutangazwa notisi ya kusitisha
kufanyika maendelezo kwenye vijiji vinavyozunguka Mgodi wa North Mara vya
Kemorera na Kewanja vilivyopo wilayani Tarime na Mkuu wa wilaya Mtemi Msafiri.
Evelyne alisema, wakati
mchakato wa kutwaa eneo kwa ajili ya shughuli za uchimbaji madini ukifanyika
tayari baadhi ya wananchi wasio waaminifu katika maeneo ya Nyamongo wameanza
kufanya maendelezo kwa kasi (Tegesha) kwa kupanda migomba na Mialovela lengo likiwa
kujipatia fedha wakati wa zoezi la uthamini.
‘’Wananchi mmekosa
subira kabisa mmeanza kupanda mialovera, migomba, miembe na katani ili mjipatie fedha huko ni
kutegesha na serikali haiko tayari kuwalipa watu wa aina hiyo, mimi kama
mshauri wa uthamini nasema ni kosa kufanya hivyo’’ alisema Evelyne
Amewataka wananchi wa
wameneo hayo hasa wanawake kutodanganywa kwa kushiriki kupanda vitu kwa
kutegesha kwa kuwa havitahesabiwa na badala yake wote waliofanya hivyo waondoe walivyoapanda
ili kuepuka hasara ya kutolipwa.
Akitangaza uamuzi wa
kusitisha maendeleo kwenye eneo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime Injinia Mtemi
Msafiri alisema kuanzia siku ya kutangazwa notisi ya usitishaji hairuhusiwi mtu
yoyote kufanya maendelezo na wananchi ambao vijiji vyao vinapitiwa na zoezi
hilo wanatakiwa kusubiri zoezi la uthamini na atakayeenda kinyume atahesabika kama
ametegesha
Alisema, Mgodi wa
Dhahabu wa Barrick North Mara sasa unamilikiwa kwa ubia wa Kampuni ya Barick na
Serikali kupitia Twiga Corporation Ltd na kusisitiza udanganyifu utakaofanyika
utasababisha wananchi kutolipwa kwa wakati kama ilivyotokea kwenye zoezi la
awali lililolazimu kufanyika uhakiki katika maeneo yaliyothaminiwa.
Kwa mujibu wa Mrakibu
wa Maendeleo ya Jamii wa Mgodi wa Barrick North Mara Sadala Hamis eneo
linalotakiwa kuchukuliwa kwa shughuli za uchimbaji madini kwenye vijiji
vinavyozunguka mgodi huo lina ukubwa wa takriban hekta 404 na wakazi
wasioopungua mia tatu.
Hivi karibuni wakati wa
kutoa fidia ya shilingi bilioni 33 kwa wakazi 1,639 wa vijiji vya Matongo na
Nyabichune katika eneo la Nyamongo Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazo Dkt Angeline Mabula alieleza kuwa zoezi la utoaji fidia lilichukua muda
mrefu kwa sababu wananchi hawakuwa wakitoa taarifa sahihi na baadhi kutegesha
na kuwaasa kutoa ushirikiano na kuwa wakweli katika masuala yanahusu ulipaji
fidia sambamba na kuwataka kutowekeza
maeneo ambayo mgodi unataka kuyachukua.
No comments:
Post a Comment