HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 08, 2020

Ametua

Kocha Mkuu wa mabingwa wa kihistoria Tanzania Yanga SC, Luc Eymael.

Na Mwandishi Wetu 

HATIMAYE Kocha Mkuu wa mabingwa wa kihistoria Tanzania Yanga SC, Luc Eymael alitua jana nchini tayari kwa ajili ya kukiongoza kikosi cha Wananchi kumalizia msimu huu.

Kocha Luc alikwama nchini kwao kwa takribani wiki mbili baada ya Ligi kurejeswa Jambo ambalo liliibua sintofahamu nzito katika mitaa ya Twiga na Jangwani.

Licha ya kuibua sintofahamu lakini Kocha huyo alionyeshwa kukerekwa na jinsi ambavyo klabu yake haikuchukua hatua za haraka kuhakikisha anarejea haraka kukiandaa kikosi  kwa ajili ya michezo ya Ligi na Kombe la Azam Sports Federation Cup.

Luc alitua jana jijini Dar es Salaam akiwa na mkewake Patricia Eymael ambaye alifunga nae pingu za maisha siku za hivi karibuni nyumbani kwako Ubelgiji.

Kwa mujibu wa taarifa za awali Luc alitakiwa kuwasili nchini wiki mbili zilizopita jambo ambalo halikuwezekana kutokana na Uongozi wa Yanga kushindwa kumtumia tiketi kwa wakati.

Licha ya hivyo, hata walipomtumia tiketi walituma moja kiasi cha kumfanya ashindwe kurejea juma moja lililopita kwani alipaswa kurejea na mkewe Patricia.

Wiki iliyopita alinukuliwa Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Kampuni ya GSM ambao ndio wadhamini wa klabu hiyo Hersi Said kuwa Kocha atatua muda wowote kwani walikuwa wakipambana kuhakikisha anarejea haraka iwezekanavyo.

Baada ya kutua Kocha Luc tayari ameshajiunga na timu na leo atakuwa anaongoza mazoezi ya vijana wake katika VIwanja vya Chuo cha Sheria jijini Dar es Salaam.

Luc anakabiliwa na kibarua kizito cha kuhakikisha wanapata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Kimataifa msimu ujao ambapo kama sio kuwa Mabingwa wa Ligi Kuu basi inabidi kuchanga karata zake vema katika kombe la FA.

Ukiondoa mechi 11 za VPL walizonazo Wananchi pia kuna dakika 270 za FA ambapo wanapaswa kuzitumia kumpata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Kimataifa msimu ujao 2020/21.

Katika dakika hizo 270 tayari 90 zimeshaangukia kwa Wana Nkurunkumbi Kagera Sugar hatua ya robo fainali ya kombe hilo.

No comments:

Post a Comment

Pages