HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 06, 2020

CHADEMA YAFUNGUA MILANGO WANAOWANIA NAFASI YA RAIS WA ZANZIBAR

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Zanzibar, Salum Mwalim, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Zanzibar leo, kuhusu kusudio la chama hicho kusimamisha mgombea katika nafasi ya Rais wa Zanzibar katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu. (Na Mpiga Picha Wetu).



Na Mwandishi Wetu, Zanzibar


Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza kusudio la kusimamisha mgombea katika nafasi ya Urais wa Zanzibar katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu na hivyo inafungua milango kwa wanachama wake wenye sifa kutangaza nia.

Hii ni mara ya kwanza kwa CHADEMA kutangaza rasmi kuweka mgombea katika nafasi hiyo ya juu ya nchi kwa upande wa Zanzibar.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar Salum Mwalim ametoa tangazo hilo katika mkutano na waandishi wa Habari uliofanyika leo Jumamosi June 06, 2020 katika Ofisi Kuu ya Chadema , Kisiwandui Zanzibar.

“Tunawatangazia rasmi wanachama wetu wenye nia ya kugombea nafasi ya Rais wa Zanzibar waandike kwa Katibu Mkuu wa chama na kuwasilisha barua hizo Ofisi ya Makao Makuu Zanzibar wakati wowote kuanzia leo hadi Juni 15, 2020 Saa Kumi na Nusu Alasiri”

“Chama kimejipima na kutafakari kwa kina na kimeona kwamba sasa ni wakati mufaka kuwapa nafasi wanachama wake wenye ndoto na uwezo wa kugombea nafasi hiyo kutimiza ndoto zao” 

Kwa sasa ni kutanga kusudio la nia zao kwa chama na kwamba baada ya hapo utafuata mchakato wa uchukuaji wa Fomu za ndani ya chama ambapo maelekezo yake pamoja na utaratibu mzima utakaofuata utatolewa baadae. 

Kwa watakaowasilisha taarifa zao wataruhusiwa kutangaza kusudio lao hilo kwa Umma kupitia vyombo vya habari.
“Niwaombe wanachama wetu wenye Sifa, Vigezo na Maadili ya chama kama yalivyoelekezwa katika Sura ya Kumi ya Kanuni kwenye katiba ya Chama ya Mwaka 2006  toleo la 2019  na matakwa ya Katiba ya Zanzibar kujitokeza.”

Niwatake wanachama wetu wote kufuguliwa kwa mlango huu usiwe chanzo cha kuvuruga umoja na mshikamano ambao umekuwa thabiti ndani ya chama chetu Zanzibar
Pamoja na tangazo hili, chama chetu kipo tayari kuendeleza ushirikiano na vyama na kulinda nia na shabaha ya ushirikiano huo bila kuathiri malengo ya vyama vyetu kwa masilahi ya kila M-Zanzibari katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba.

Aidha, tunaendelea kuwasisitiza wanachama wetu walioonesha nia ya kugombea nafasi za Udiwani, Uwakilishi na Ubunge kwa Unguja na Pemba kuendelea  na taratibu za chama  na kwamba milango bado ipo wazi kwa ambao bado hawajafanya hivyo.  

Chama kinawatakia kheri wanachama wake, pamoja na wafuasi na wapenzi  na kwa pamoja tunawataka kuendelea kujipanga kukiletea chama ushindi katika uchuguzi Mkuu wa Oktoba .

No comments:

Post a Comment

Pages