HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 27, 2020

Polisi wavunja mkutano wa THRDC, wawili wahojiwa

Na Janeth Jovin

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limevunja mkutano wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) na kuwakamata wafanyakazi wawili wa mtandao huo.

Hata hivyo THRDC umesema kuwa umesikitishwa na  unalaani vikali kitendo cha ukamatwaji wa wafanyakazi hao wawili wa THRDC, ambao ni Remmy Lema, Meneja Programu wa THRDC pamoja na Wakili Catherine Ringo - Ofisa Utetezi wa THRDC  mapema asubuhi ya jana.

Katika taarifa kwa vyombo vya ahabri iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na mtandao huo, ilieleza kuwa saa 2:30 asubuhi, askari wa Jeshi wa Polisi walifika kwenye  ukumbi wa mkutano maeneo ya Millenium Towers kwenye ukumbi wa Kisenga LAPF, ghorofa ya 14 ambapo mtandao huo ulikuwa umeandaa kuendesha mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo wanachama wake wapya 30 juu ya usalama na tathmini ya hatari.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa hapo awali, wafanyakazi hao wawili waliitwa na polisi kwa mahojiano na baadaye kuondoka nao kuelekea kituo cha Polisi cha Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, taarifa hiyo ilieleza kuwa  miongoni mwa kundi hilo la maaskari ni mmoja tu aliyekuwa kwenye mavazi ya Jeshi la Polisi huku wengine wote wakiwa wamevaa nguo za kiraia.

"Aidha, muda mfupi baada ya kuwachukua wafanyakazi hao, askari wengine watatu wa Jeshi la polisi walikuja ukumbini na kuwaamuru wafanyakazi waliobakia kusitisha mafunzo hayo.

"Baada ya mawakili wetu wawili; Wakili Jones Sendodo na Wakili Shilinde Swedy wa THRDC kufuatilia tukio hili la kiusalama katika kituo cha Polisi cha Oysterbay, hatimaye polisi wamewaachia huru wafanyakazi hao wawili," ilieleza taarifa hiyo.

Ilieleza kuwa katika mahojiano mafupi yaliyofanyika kati ya mawakili wao na askari hao wa Jeshi la Polisi katika kituo cha Oysterbay, polisi wamedai kuwa ni lazima wasitishe mafunzo hayo kwakuwa yanakiuka sheria za nchi licha ya kutotaja  Sheria hizo.

"Katika hali ya kushangaza, polisi wamehoji kwanini tunaendesha mafunzo yetu bila ruhusa ya Jeshi la Polisi na bila ajenda yetu kukaguliwa na polisi, jambo ambalo ni kinyume kabisa na uhuru wa uendeshaji wa kazi za Asasi za Kiraia. Ni dhahiri huu ni mwendelezo wa uminywaji wa nafasi ya asasi za kiraia pamoja na uhuru wa kukutana," ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa THRDC umekuwa ukiendesha mafunzo hayo kama sehemu ya kazi zake za utetezi kwa miaka saba sasa bila kuvunja sheria za nchi tangu mwaka 2013.

Hata hivyo, alisema hiyo ni mara ya pili kwa tukio kama hili kujitokeza. "Itakumbukwa kuwa, mara ya kwanza mnamo Juni 3 mwaka 2017,  Bw. Onesmo Olengurumwa - Mratibu Kitaifa wa THRDC naye alikamatwa na polisi katika maandalizi ya mkutano wetu mwingine," .

Aidha taarifa hiyo iloeleza kuwa Kwa sasa wamelazimika kusitisha mafunzo kwa muda huku wakiendelea kufuatilia muafaka wa suala hilo katika kituo cha Polisi Oysterbay.

No comments:

Post a Comment

Pages