Mkuu
wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina, akimuongoza Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor
Mpango (Mb), kukagua jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, alipotembelea
na kukagua ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa
Wilaya ya hiyo, Mkoa wa Kigoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip
Isdor Mpango (Mb) (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa
Wilaya ya Buhigwe na mafundi wanaojenga Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya hiyo baada
ya kukagua jengo hilo mkoani Kigoma. (Picha na Josephine Majura – KIGOMA).
Na Josephine
Majura na Peter Haule KIGOMA
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt Philip Isdor
Mpango (Mb), ameupongeza uongozi wa mkoa wa Kigoma na Wilaya ya Buhigwe kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa Ofisi ya
Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe inayojengwa katika eneo la Bwega, Tarafa ya Manyovu,
wilayani Buhigwe mkoani Kigoma na kuagiza Jengo hilo likamilike kabla ya mwezi
wa kumi ili wananchi wa wilaya hiyo waanze kupata huduma kwenye jengo hilo
jipya.
Dkt. Mpango ametoa pongezi hizo alipotembelea na
kukagua ujenzi wa jengo hilo jipya la Ofisi ya MKuu wa Wilaya mpya ya Buhigwe
ambalo hadi kukamilika kwake litagharimu shilingi bilioni 1.1
“Nakupongeza Mkuu wa Wilaya na timu yako yote kwa
usimamizi mzuri wa Fedha za Serikali, lazima tujenge Makao Makuu ya Wilaya
ambayo yataishi kwa miaka mingi, kwa hiyo nimefurahi jengo ninavyoliona hata
kama sio Mhandisi lakini ninaona lina ubora”. alisisitiza Dkt. Mpango.
Alimtaka Mkuu wa Wilaya kuendelea kusimamia rasilimali
fedha zinazotolewa na Serikali kama
alivyofanya kwenye mradi wa ujenzi wa
Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ili thamani ya fedha za miradi inayotekelezwa
ilingane na thamani ya fedha zilizotolewa.
Kwa upande wake, Meneja mradi huo Masawika Kachenje, akisoma
taarifa ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe amesema kuwa hadi
sasa kiasi cha shilingi milioni mia tano (500,000,000) ambazo Serikali zilitoa
kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huo kimetumika kukamilisha awamu ya kwanza ya
ujenzi.
Aliongeza kuwa kiasi cha shilingi milioni (550,000,000),
kimebaki ili kukamilisha kiasi cha sh. Bilioni 1.1 ikiwa ni gharama ya utekelezaji
wa mradi wa ujenzi jengo zima, ambapo mipango ya Wilaya ilikuwa
kukamilisha ujenzi huo ifikapo mwezi Julai tarehe 15 mwaka 2020.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali,
Michaeli Ngayalina, amemshukuru Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango,
kwa kutembelea na kukagua baadhi ya miradi inayotekelezwa kwa Fedha za Serikali
na kuahidi kuzisimamia vizuri fedha zote zinazotolewa na Serikali kukamilisha
miradi ya maendeleo.
Kanali Ngayalina, amemuomba Dkt. Mpango kusaidia
upatikanaji wa Fedha zilizobaki ili waweze kukamilisha ujenzi wa ofisi hiyo
kama ilivyopangwa kwenye ratiba.
No comments:
Post a Comment