>Wanakijiji
wahofia miujiza ya Msitu wa Mbumbila kupotea
Ofisi ya Kijiji cha Nanjilinji A wilayani Kilwa mkoani Lindi ambayo
imejemgwa kwa shilingi milioni 70 fedha kutoka Msitu wa Mbumbila ikiwa
ni mafanikio ya USMJ.
Mkuu
wa Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, Christopher Ngubiagai, akizungumza na
waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu manufaa ya USMJ katika vijiji
vyake 13.
Katibu
wa Kamati ya Maliasili Kijiji cha Nanjilinji A wilayani Kilwa mkoani
Lindi akitoa taarifa ya miaka minne ya kijiji hicho kuhusu manufaa ya
USMJ kwa waandishi wa habari.
Mkazi wa Kijiji cha Nanjilinji A wilayani Kilwa mkoani Lindi, Mosi Yassin, akieleza kwa waandishi wa
habari alivyonufaika na shilingi 50,000 ya wakati anaenda kujifungua
fedha zinatokana na USMJ.
NA SULEIMAN MSUYA
SHERIA ya Misitu ya
mwaka 2002, Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya
mwaka 1999, Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) ya mwaka 1982 (na
marekebisho yake), Kanuni za Misitu (uzalishaji wa mkaa, usafirishaji na
uuzaji) ya mwaka 2006 na Kanuni za Misitu za mwaka 2004 ni moja ya nguzo muhimu
katika ulinzi na usimamizi wa rasilimali misitu nchini.
Misitu ni mkusanyiko wa
miti mbalimbali ya asili na isiyo asili ambayo ipo katika maeneo ya mijini na
vijijini ambayo huchangia upatikanaji wa hewa safi, mvua, mazingira bora na
mengine mengi.
Mnamo Mei 24, 2019,
Serikali ya Tanzania ilipitisha Kanuni za Misitu za (Utumiaji endelevu wa
magogo, mbao, fito, nguzo au mkaa) za mwaka 2019, Tangazo la Serikali la 417.
Tangazo hilo la
Serikali (GN 417), pamoja na kuonesha nia njema katika dhana nzima ya
kuhakikisha misitu inakuwa endelevu kwa upande mwingine linaonekana kuenda
kuuwa dhana nzima ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu Jamii (USMJ) na Biashara ya
Endelevu ya Mazao ya Misitu (FBE) hasa vijijini.
Kuna wasiwasi
unaojitokeza kuhusu madhara ya kanuni hizi kwa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya
Jamii. Kusudi la Makala hii ni kuonyesha kwa muhtasari mabadiliko yaliyoletwa
na Kanuni hizi na kuainisha athari zitakazojitokeza kwa USM hasa vijijini.
Wasiwasi wa kanuni hizo
mpya unaoneshwa na wanavijiji na halmashauri ambazo zinazingatia dhana ya USMJ
na kuifanya rasilimali misitu kuwa na matokeo chanya kwa vijiji, wanavijiji na
halmashauri kwa ujumla.
Kanuni hizi
zinatofautiana na Sheria ya Misitu na Kanuni zingine zilizopita kwa namna
mbalimbali zifuatazo kwa kuhamisha wajibu wa kuandaa mipango ya uvunaji katika
Misitu ya Hifadhi za vijiji kutoka kwa Halmashauri ya kijiji kwenda kwa
Mkurugenzi wa Misitu.
Mabadiliko hayo
yanapingana na Sheria ya Misitu ya mwaka 2002 ambayo inatamka kwamba halmashauri
za vijiji zina wajibu wa kuandaa mipango ya usimamizi wa misitu ya hifadhi za
vijiji.
“Hii inajumuisha
kupanga kwa ajili ya uvunaji na matumizi endelevu kwenye hifadhi ya misitu ya
vijiji. Haki ya halmashauri za vijiji kuamua juu ya namna ya kusimamia ardhi ya
vijiji na misitu iliyoko kwenye ardhi ya vijiji imeelezwa katika Sheria ya
Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999 na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka ya
Wilaya) ya mwaka 1982.
Kanuni za mwaka 2019
zinahamisha wajibu wa kuandaa mipango ya uvunaji katika ardhi za vijiji kwa
Mkurugenzi wa Misitu.
Pia mamlaka ya kufanya
maamuzi juu ya utumiaji wa misitu iliyoko kwenye ardhi za vijiji yametolewa
kutoka kwa halmashauri ya kijiji na kupewa Mkurugenzi wa Misitu,”.
Kanuni hizi zinakinzana
na kwenda kinyume na ‘Sheria mama’ Sheria ya Misitu ambayo inatoa mamlaka ya
kufanya maamuzi kwa halmashauri za vijiji.
Kanuni hizi zimeenda
kinyume na Sheria ya Ardhi za Vijiji ya mwaka 1999 ambayo pia inatoa mamlaka ya
kufanya maamuzi juu ya usimamizi wa ardhi za vijiji kwa halmashauri za vijiji.
Kanuni hizi zinaenda
kinyume na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka ya Wilaya) ya mwaka 1982 ambayo
inatoa haki kwa halmashauri za vijiji kupitisha sheria ndogo za mambo yote na
shughuli zote ndani ya kijiji.
Kanuni hizi pia
zinakinzana na Sera ya Taifa ya Misitu amabyo inabainisha usimamizi shirikishi
wa Misitu kama nyenzo ya kisera kwa ajili ya usimamizi wa misitu iliyoko kwenye
ardhi za vijiji.
Aidha, uamuzi wa kuhamisha
wajibu wa kutoa vibali vya uvunaji kwenye misitu ya hifadhi za vijiji kutoka
kwa halmashauri ya vijiji kwenda kwa Kamati ya Wilaya ya Uvunaji wa Mazao ya
Misitu.
Sheria ya Misitu ya
mwaka 2002 inatamka kwamba halmashauri za vijiji zinawajibu wa kusimamia misitu
ya hifadhi iliyoko kwenye ardhi za vijiji.Hii ni pamoja na kutoa vibali vya
uvunaji katika Hifadhi za Misitu iliyoko kwenye ardhi za vijiji.
Kanuni za mwaka 2019
zinahamisha wajibu wa kutoa vibali vya uvunaji katika misitu ya hifadhi iliyoko
kwenye ardhi za vijiji (na katika ardhi yote ya vijiji) kwa Kamati ya Wilaya ya
Uvunaji wa Mazao ya Misitu.
Pia yapo mabadiliko
mengine ya kikanuni ambayo kwa ujumla wake yanapelekea wakati mgumu kwa vijiji,
wanavijiji na halmashauri ambazo zinamiliki misitu kuwa katika wakati mgumu wa
kuamini dhana ya USMJ kuendelea.
Taarifa za mabadiliko
ya kanuni yaani GN 417 yanawatia hofu wanakijiji na viongozi wa Kijiji cha
Nanjilinji A, Kata ya Nanjilinji Tarafa ya Nanjilinji wilayani Kilwa mkoani
Lindi ambao wanaamini USMJ na FBE imesababisha kutokea miujiza ya kiuchumi,
huduma za jamii na maendeleo kijijini kwao.
VIONGOZI,
WANAKIJIJI NANJILINJI
Ofisa Mtendaji wa
Kijiji cha Nanjilinji A, Muhidini Mkunguru anasema kijiji chake kina watu 3,303
kaya 892 ambapo USMJ na FBE imeanza 2012 kwa mara ya kwanza kupitia Shirika la
Kuhifadhi Mpingo na Maendeleo (MCDI).
Anasema ujio wa MCDI
ulikutana na changamoto nyingi kwa wananchi kukosa imani na wageni hao
wakiamini kuwa ni matapele lakini elimu ilivyotolewa walikubali na kuwaruhusu
kufanya kazi ambapo sasa kuna manufaaa makubwa.
“MCDI wamekuja hapa
tulikuwa tunakusanya mapato kwa mawaka yasiyozidi shilingi milioni 30 lakini
kwa sasa tunaingia zaidi ya shilingi milioni 100 huu ni muujiza unaotoka Msitu
wa Mbumbila,” anasema
Mkunguru anasema
miujiza ya Misitu wa Mbumbila umefanikisha ujenzi wa shule ya msingi, nyumba ya
mwalimu, ofisi ya kijjiji yenye thamani ya shilingi milioni 70, nyumba ya
kulala wageni yenye thamani shilingi milioni 107, wanafunzi zaidi ya 400
waliofaulu wamepatiwa shilingi laki moja kila mmoja, wakina mama wajawazito
wanapatiwa shilingi 50,000 wakikaribia kujifungua jambo ambalo linaweza
kutoweka kupitia GN 417.
“Ninavyosema Msitu wa
Mbumbila ni muujiza ndani ya Kijiji cha Nanjilinji A namaanisha miujiza kweli
kwani zaidi ya milioni 850 zimepatikana na hili limetimia baada ya kupatiwa
elimu ya USMJ, FBE na MCDI huko nyuma hatukuona Serikali Kuu ikirejesha faida
kwa vijiji ndio maana nasema siwezi kuunga mkono hiyo GN mpya kama haitakuja
kwa mfumo huu,” anasema.
Mtendaji huyo anasema iwapo
Serikali itakuja na wazo la kuhamishia usimamizi wa misitu Serikali kuna huduma
nyingi zitakwama lakini pia misitu haitakuwa salama.
“Hapa tunashuhudia
misitu ambayo ipo chini ya TFS inaharibiwa na hakuna hatua muhimu zinachukuliwa
hivyo ni vema Serikali ikatafakari vema kanuni zake mpya ili misitu iweze kuwa
endelevu,” anasema.
Mwenyekiti wa Kijiji
cha Nanjilinji A, Mohammed Mussa anasema amani na maendeleo ambayo yanapatikana
kijijini kwao imetokana na miujiza ya Msitu wa Mbumbila baada ya wanakijiji
kuelewa maana ya USMJ na FBE.
Mussa anasema USMJ na
FBE kupitia MCDI imesadia kupunguza migogoro ambayo ilikuwa inatokea kati ya walinzi
wa misitu, wafugaji na wakulima.
“Mimi kama kiongozi
wakuchaguliwa na wananchi nimekuwa nikitekeleza majukumu yangu na wananchi bila
itikadi za kidini, siasa, kabila na
rangi kwa kuwa maendeleo yanaonekana na
kichocheo kikubwa ni USMJ na FBE,” anasema.
Katibu wa Kamati ya
Maliasili Kijiji cha Nanjilinji A, Said Bakari anasema ubora na uendelevu wa
misitu umechangiwa na jamii kuamua kuulinda kwa nguvu zote hivyo kutoa angalizo
kwa Serikali kujirishidha kabla haijafanya maamuzi yoyote.
“Kila mwananchi ni
mlinzi wa msitu na sababu kubwa ni zawadi ya shilingi 100,000 kwa yoyote ambaye
atatoa taarifa za uharibifu unaofanywa jambo ambalo TFS wameshindwa kulifanya
kwa asilimia kubwa,” anasema.
Anasema iwapo Serikali
inaona hiyo ndiyo njia sahihi ya kurejesha usimamizi katika ngazi ya Serikali
Kuu hawawezi kuzuia kwani hayo ni mamlaka yao ila athari za mazingira, uchumi, maendeleo
na jamii zitatokea.
Naye Mosi Yassin
anasema miujiza mingine ya Msitu wa Mbumbila katika USMJ na FBE ni kumfanya
mama aone mimba ni fursa na sio kwani Nanjilinji A kijiji kizima kinahusika na
mimba hiyo jambo ambalo haliwezi kufanywa na Serikali.
“Hapa kwetu kupitia
Msitu wa Mbumbila tunafurahia ndoa na kuzaa watoto kwani huko zamani hatukupata
huduma hii ya kupewa shilingi 50,000 wakati wa kujifungua, yaani Nanjilinji uzazi
salama ni shirikishi na msingi mkubwa ni USMJ na FBE kupitia elimu ya MCDI,”
anasema
DFO
KILWA
Kwa upande wake Ofisa
Misitu Msaidizi wa Wilaya ya Kilwa Achsah Ezekiel anasema USMJ na FBE imeweza
kuchochea uendelevu wa misitu katika vijiji husika hivyo Serikali Kuu kuja na
mtazamo wa kurejesha usimamizi katika ngazi ya kitaifa ni hatari kwa kuwa
hakuna rasilimali za kutosha za kusimamia misitu.
“Mfano Kijiji cha
Nanjilinji A ambacho kimeamua kusimamia misitu kwa dhana ya shirikishi kuna
huduma za kijamii na miradi ya maendeleo imetekelezwa huku USM ikionekana ndani
ya msitu jambo ambalo Serikali Kuu haitaweza,” anasema.
Ezekiel anasema iwapo
Serikali inataka kuja na kanuni ambazo zitajerejesha mamlaka ya USMJ Serikali
Kuu ni vema ikajikita katika elimu zaidi ili haya ambayo yanaonekana sasa yawe
endelevu.
“Vijiji kama vya
Liwiti, Likawage, Kikole, Ngea, Mchakama, Kipitimbi, Nanjilinji na vingine
vimetekeleza USMJ na FBE mabadiliko ni makubwa ya kiuhifadhi,” anasema.
TFS
KILWA
Mhifadhi wa Misitu wa
TFS Kilwa, Abbas Ntandu anasema ufanisi wa TFS unahitaji kufanyakazi na
wanavijiji ili kuziba pengo la watumishi hali ambayo inawasaidia kupata taarifa
mapema za uharibifu.
Anasema hoja ya
kurejesha usimamizi wa misitu Serikali Kuu inaweza kuharibu misitu au kuboresha
iwapo mambo ya msingi hayatazingatiwa.
Mhifadhi huyo anasema
kinachohitajika ni kuwa na taasisi moja ambayo itaweza kusimamia rasilimali
hiyo kwa pamoja kwa kuangalia maslahi ya wananchi na nchi.
“Ni sisi kutoa elimu
tukiwa wamoja tofauti na ilivyo sasa ambapo kunaonekana kuwa kila mtu
anapigania eneo lake huku elimu kwa wananchi ikiwa bado haijafika,” anasema.
Ntandu anasema dhana
hiyo haihitaji kuwanyang’anya wanavijiji bali ni kuangalia namna kila mwananchi
anaweza kunufaika na rasilimali misitu na hayo yote yatatoa matokeo chanya kama
elimu itatolewa.
MCDI
Akizungumzia GN hiyo na
dhana ya USMJ na FBE, Meneja Uthibitishaji Misitu wa MCDI, Glory Masao anasema
wanavijiji wenye misitu wameonesha moyo wa kuilinda baada ya kunufaika hivyo
kutaka kuhamisha mamlaka kunaweza kuchangia uharibifu.
“Sisi tumeamua kutoa
elimu na kuonesha namna jamii inavyoweza kulinda rasilimali zake pale
inaponufaika hivyo Serikali ikija na wazo jingine hatuna budi kufuata lakini
lazima tuwe na hofu ya uendelevu,” anasema.
DAS
KILWA
Katibu Tawala (DAS)
Wilaya ya Kilwa, Haji Balozi anasema wilaya hiyo ambayo ina vitongoji 351vijiji
90, kata 23 ila vijiji vichache ambavyo vimejikita katika USMJ na FBE
vimeonesha athari chanya ya kuwepo mfumo huo wa usimamizi wa misitu shirikishi.
Balozi anasema miujiza
inayotekea Kilwa kupitia misitu inapaswa kuambukizwa kila wilaya ambapo vijiji
vyake vinarasilimali misitu na sio kufikiria kurejesha Serikali Kuu.
“Inawezeka lengo la
Serikali ni zuri lakini inatakiwa kutafakari kwa kina kwani mfumo wa USMJ na
FBE sisi kama sehemu ya wawakilishi wa Serikali tunaona unafaa kinachohitajika
ni maboesho ambayo yataweza kuleta tija zaidi,” anasema.
DAS Balozi anasema
dhana ya USMJ na FBE imechochea kuwepo mifumo sahihi ya kiungozi kwenye vijiji
vyenye misitu hivyo ni Imani yake kama angeona Serikali inakuja na mawazo ya
kuiboresha zaidi na sio kuja na kanuni ambazo zinaweza kuchochea uharibifu.
DED
KILWA
“Hatuombei hili la
uchukuaji usimamizi wa misitu ya vijiji litokee kwani sisi Kilwa tunatambua
faida yake,” hayo ni maneno ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilwa Renatus Mchau
wakati akizungumza na mwandishi sa Makala hii ofisi kake.
Mchau anasema pamoja na
changamoto ambazo zipo USMJ na FBE imechochea maendeleo na uhifadhi kwa
asilimia kubwa tofauti na zamani ambapo misitu yote ilikuwa inasimamiwa na
Serikali Kuu.
“Ni wapi utaenda ukute
misitu imetumika kujenga ofisi ya kijiji boa kuliko hii ya kwangu, nyumz ya
kulala wageni, shule, wazazi kupewa fedha za kujifungulia na watoto kununuliwa
sare za shule narudia bila USMJ na FBE ni ngumu kuona vitu kama hivi,”anasema.
DC
KILWA
Mkuu wa Wilaya ya
Kilwa, Chritopher Ngubiagai anasema Kilwa ina misitu ya asili yenye ukubwa wa
hekta 600,000 na kilimo hekta 300,000 hivyo dhana ya usimamizi shiriki ndio
inaweza kuifanya misitu hiyo kuwa endelevu.
Ngubiagai anasema
vijiji 13 ambavyo vipo kwenye miradi mbalimbali ikiwemo ya MCDI vimekuwa na
matokeo chanya ya USMJ hivyo ni jukumu la Serikali kuu kuendeleza dhana hiyo
ambayo ina manufaa ya kiuchumi, kijamii na maendeleo.
“Mimi naona anguko la
kichumi, kijamii, maendeleo na mazingira iwapo USMJ na FBE itatoka kwa vijiji
na kuhamia Serikali Kuu kwani huu uendelevu wa misitu ambao tunaringia Kilwa
umtokana na jamii kunfaika na misitu yake kinyume na hapo ni janga,” anasema.
Ngubiagai anasema
kinachoweza kutokea baada ya vijiji kukosa mamlaka kupitia hiyo kanuni mpya ni
kuongezeka kwa gharama za usimamizi na faida kuwa ndogo jambo ambalo
halipendezi.
“Kwa sasa wananchi
wanachukulia misitu hiyo ni mali yao, hivyo wana uchungu nao na hali hiyo
imejengwa na wadau kama MCDI, TFS, Mtandao wa Jamii waUsimamizi wa Misitu
Tanzania (MJUMITA), Shirika la Kuhifadhi Misitu Tanzania (TFCG), Shirika la
Kuendeleza Nishati Tanzania (TaTADO), hamashauri na wengine wengi,” anasema.
TFS
Akijibu maswali kuhusu
namna gani TFS inafuika USMJ na FBE, Kamishna Mhifadhi Misitu, Profesa Do
Santos Silayo anasema katika kuhakiksha msitu inalindwa vizuri ushiriki wa
wananchi wanaoishi kuzunguka misitu ni
wa umuhimu mkubwa.
Anasema hata hivyo ili
wananchi washiriki katika uhifadhi wa misitu hiyo wanapaswa kuona faida kutoka katika misitu
hiyo wanayoshiriki kuitunza.
“Misitu ina faida
nyingi zikiwepo za moja kwa moja
zinazohusu kuvuna miti lakini pia zipo za kimazingira ikiwapo uhifadhi wa vyanzo vya maji, ufugaji wa nyuki na utunzaji
wa hali ya hewa.
Moja ya mkakati ambao
TFS inatumia kuwashirikisha wananchi
kwanza ni kutoa elimu kwa
wananchi ili waelewe kuwa faida za misitu zipo nyingi na sio
mbao na mkaa tu. Hii huwafanya waone fursa nyingine zinazoweza
kupatikana ikiwa misitu inayowazunguka itatunzwa vizuri,” anasema.
Prof. Silayo anasema baadhi
ya fursa ambazo TFS imewezesha wananchi ni pamoja na ufugaji wa nyuki. Pia TFS
imekuwa ikitoa misaada mbalimbali kwa
vijiji hivyo ikiwa ni pamoja na
kuvisaidia vijiji kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi na kutenga misitu ya vijiji.
Aidha, anasema TFS
imekua ikigawa miche bure kwa wananchi ili waanzishe mashamba au vijishamba
vidigo vidogo vya miti inayokua haraka kwa lengo la kujipatia kipato na mahitaji mengine ya mazao
ya misitu lakini pia kupunguza matumizi ya mazao ya misitu kutoka misitu ya
asili.
“TFS inaamini kuwa ushiriki
wa wananchi kupitia kamati za maliasili
za vijiji ni muhimu sana katika kulinda
misitu ikiwa zitaelimishwa na kuratibiwa vizuri. Kamati hizi zinaweza kwa kiasi kikubwa kulinda misitu
iliyoko karibu na vijiji vyao.
Suala muhimu ni elimu
na uwazi kwa kuwashirikisha ipasavyo katika maamuzi na hasa kuhusu
faida zitokazo na misitu wanyopaswa kuilinda. Kwa misitu inayoruhusu
uvunaji wananchi wanaweza kupata faida za moja kwa moja kutokana na mazao
yanayovunwa,” anasisitiza.
Kamishna huyo anasema hata
hivyo tatizo kubwa ni ushirikishwaji katika misitu isiyoruhusu uvunaji misitu
ambayo ni kwa ajili ya uhifadhi wa
mazingira. Katika misitu hii ushirikishwaji umeimarishwa kwa kusaidia wananchi kuanzisha miradi mbadala ya
kiuchumi kama ufugaji wa nyuki juhudi
ambazo zimeonyesha mafanikio katika
kuhifadhi misitu hiyo.
Kuhusu kanuni namba 417
kuonekana kuondoa mamlaka kwa vijiji katika mchakato wa kuvuna Silayo anasema
kwa mujibu wa sheria ya misitu mkurugenzi wa misitu amepewa malaka kusimamia
msitu yote hapa nchini.
“Tangazo la serikali Na
417 kama mwenyewe ulivyosema linalenga
kuboresha usimamizi na uendeleza wa misitu kwa kusisitiza umuhimu wa kuwa wa mipango ya usimamizi misitu na kuzuia
uvunaji holelal wa misitu.
Kwa mamlaka aliyopewa
kwa mujibu wa sheria mkurugenzi wa
misitu anapaswa kuidhinisha mipango ya uvunaji ambayo itakuwa imeandaliwa na
wamiliki wa msitu sharia kanuni na miongozo,” anasema.
Anasema kwa kuhakikisha
kuwa mipango hiyo inafuata mwongozo kuapelekea kuwepo kwa uvunaji wa mazao ya
misitu wananchi na wamiliki hawapaswi
kuwa na woga kwani mkurugenzi anaizinisha
mipango ya usimamizi wa misitu kuhakikisha inakidhi matakwa ya kisheria
unazingatia muongozo kabla ya kuruhusu
uvunaji.
“Wajibu huu
hauwapokonyi wananchi malaka ya matumizi ya msitu wao bali unawataka watimize
wajibu wao wa kuhakikisha kuwa uvunaji
unakuwa endelevu,” anasisitiza.
Pia anaongeza kuwa USMJ
na Ushirikishwaji wa Wanavijiji katika Usimamizi wa Misitu (JFM) hutumika
katika mazingira tofauti ambapo CBFM inatumika kwa misitu ya vijiji ambayo
haimilikiwi na serikali, wakati JFM
hutumika katika misitu ya serikali ambapo mmiliki ambye ni serikali huingia
makubaliano na vijiji vinavyozunguka msitu huo kusimamia msitu kwa Pamoja.
“Hivyo mifumo yote ni
sahihi kama ikisimamiwa vizuri katika mazingira yake. Hata hivyo CBFM imevutia
vijiji vingi zaidi kwa kuwa inatumika katika misitu inayomilikiwa na vijiji
vyenyewe na inasaidia kuhifadhi na
kuendeleza uhifadhi wa misitu katika
maeneo ya vijiji ambayo yalikuwa yana
changamoto ya usimamizi kwa kuwa
yalikuwa hayana kinga ya kisheria kama hifadhi.
Kwa upande wa JFM pamoja
na umuhimu wake katika kuhifadhi misitu kumekuwa na changamoto utaratibu
wa namna ya kugawana mapato yanayotoka
katika misitu inayosimamiwa kwa ubia kati ya
Serikali na wananchi na umekuwa mgumu zaidi kutumika katika misitu
ambayo malengo yake ni uhifadhi tu na hairuhusiwi kuvunwa,” anasema.
Prof. Silayo anasema katika
mazingira kama haya msisitizo umewekwa kuangalia fursa zingine zipatikanzao
ndani ya msitu lakini pia TFS imekuwa
ikisaidia katika kubuni na kuwezesha kuanzisha
miradi mbadala kama ufugaji nyuki.
No comments:
Post a Comment