HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 16, 2020

MAFUNZO YA KILIMO YALENGE KUWA CHA KIBIASHARA –KM KUSAYA

Wakufunzi wa mafunzo ya Kilimo nchini wameagizwa kufanya kazi kwa weledi kwa lengo la kuwafundisha wanafunzi kuelewa na kuwa mahili katika kilimo kibiashara.

Agizo hilo limetolewa leo Jijini Mbeya na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya alipotembelea na kuzungumza na watumishi na wanafunzi wa chuo cha Mafunzo ya Kilimo (MATI) Uyole.

Kusaya amevitaka vyuo vyote 14 vinavyotoa mafunzo ya Kilimo vya umma na vile 15 vya binafsi kuhakikisha vinawafundisha wanafunzi taaluma ya kufanya Kilimo biashara ili wakihitimu waweze kujiajili na kusaidia wakulima kuzalisha mazao kwa faida.

 “ Hiki ni chuo cha kilimo lazima tuwafundishe vizuri wanafunzi wetu ili wakitoka hapa wawe wanajua kila kitu katika sekta ya mazao ,hivyo wakufunzi wapeni nafasi wanafunzi wajifunze zaidi kwa vitendo na kutumia teknolojia rahisi” alisisitiza Katibu Mkuu huyo.

 Aliongeza kusema vyuo vyote hasa vya umma vianzishe shughuli na miradi ya kujiongezea kipato kwa kutumia ardhi na miundombinu iliyopo na kupunguza utegemezi wa bajeti ya serikali.

Katika kufikia malengo hayo ya kufundisha Kilimo cha kibiashara ,Katibu Mkuu huyo ameahidi kukichangia chuo cha MATI Uyole shilingi milioni 30 ili kiongezee katika bajeti yake kununua trekta kwa ajili ya kazi za uzalishaji mazao.

Pia amesema atakisaidia chuo hicho pikipiki tatu kwa ajili ya wakufunzi, kompyuta tano na vifaa vya TEHAMA ili chuo kianzishe maktaba mtandao (e-learning) pamoja na kuwapatia wanafunzi magunia 20 ya mpunga ili wale.

Pia ameahidi kukipatia chuo cha MATI Uyole kitalu nyumba ( Green House) kwa ajili ya wanafunzi kujifunza kwa vitendo kuzalisha mboga mboga na matunda (horticulture.

Katika kukifanya chuo hicho kinaongeza uzalishaji ameagiza uongozi wa chuo kuwasiliana na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa ajili kuanzisha miundombinu ya umwagiliaji ili kuwasaidia wanafunzi kujifunza vema kabla ya kuhitimu.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha MATI Uyole Emanuel Mwalukasa alimshukuru Katibu Mkuu huyo kwa jitihada ambazo serikali kupitia wizara ya Kilimo inafanya kuboresha mazingira ya ufundishaji.

Aidha Katibu Mkuu huyo alitembelea Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Uyole ambapo amewapongeza kwa kazi nzuri ya utafiti wa aina nyingi bora za mbegu zenye matokeo mazuri kwa wakulima.

Ameitaka taasisi hiyo kuongeza jitihada katika kufanya tafiti zenye lengo la kusaidia wakulima kuzalisha mazao mengi kibiashara na kuchangia katika uchumi wa taifa .

“Ninyi TARI mna deni kubwa kwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kufanya utafiti katika Kilimo kionekane chenye tija na kukifanya cha kibiashara na kuwezesha matokeo ya tafiti hizi za mbegu kuwafikia wakulima na maafisa ugani vijijini” alisema Kusaya.

Kuhusu maonesho ya Nanenane ameagiza taasisi zote za mafunzo ya Kilimo na utafiti siku zote kuwezesha wakulima na wananchi kujifunza kilimo na teknolojia muda wote ,hivyo elimu itolewe kwa watu wengi zaidi nchini ili kuleta mapinduzi ya kilimo.

Akiwa mkoani Mbeya Katibu Mkuu Kusaya amekagua maandalizi ya maonesho ya Nane nane katika viwanja vya John Mwakangale na kuwataka wadau wajitokeze na kuendelea na maandalizi.

Kauli mbiu ya Nanenane mwaka huu inasema “Kwa Maendeleo ya Kilimo,Uvuvi na Mifugo Chagua Viongozi Bora 2020” ambapo kitaifa maonesho hayo yatafanyika mkoani Simiyu . Katibu Mkuu Kusaya yupo mkoani Mbeya kwa ziara ya kikazi kutembelea taasisi zilizochini ya wizara yake na kuongea na watumishi ikiwa na lengo la kuongeza tija katika utendaji kazi wenye matokeo chanya kwa sekta ya Kilimo.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya (kulia) akikabidhi zawadi ya magunia ishirini ya mpunga kwa Rais wa Serikali ya wanafunzi chuo cha mafunzo ya kilimo (MATI) Uyole Baitan Sanga leo jijini Mbeya.Zawadi hiyo inalenga kuwafanya vijana hao wasome kwa bidii.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya ( kushoto) akitazama parachichi aina ya Hass zilizofanyiwa utafiti na kituo cha utafiti wa kilimo (TARI) Uyole.

No comments:

Post a Comment

Pages