HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 29, 2020

Shibuda apitishwa na ADA- Tadea kugombea urais

Na Janeth Jovin

KATIBU Mkuu wa Chama cha ADA-Tadea, John Shibuda, amepitishwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho, kugombea urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, 2020.

Akizungumza katika mkutano mkuu uliofanyika jana Jumanne Julai 28, 2020 jijini Dar es Salaam, Katibu wa Oganaizesheni ya uchaguzi wa chama hicho, Zuberi Hamis amesema mkitano huo pia umempitisha Juma Ali Khatib ambaye ni waziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar asiyekuwa na wizara maalum kugombea Urais wa Zanzibar huku Hassan Karonel Kijogoo atakuwa mgombea mwenza wa Urais wa Tanzania.

Hamis amesema wagombea nafasi ya urais wa Tanzania walikuwa wawili, Shibuda na Mastadia Hilali Munika na upande wa Zanzibar alikuwa mmoja Khatib.

Amesema wanachama waliopiga kura walikuwa 130 kati ya hizo, Shibuda amepata kura 120 na Mastadia akiambulia kura 10.

Katibu huyo amesema, Khatibu amepata kura 126 na kura nne zilipigwa hapana.

Baada ya kutangazwa mshindi, Shubuda ambaye ni mwenyekiti wa Baraza la vyama vya siasa nchini amesema, akishinda Urais wa Tanzania atahakikisha anaweka usawa kwa wananchi ikiwemo kuendesha shughuli za umma pasina upendeleo wa aina yoyote.

Naye, Khatibu amesema atahakikisha wanawake wanaoishi mazingira magumu hususan wanaopata mimba na wale wenye tabia za kuwakimbia waume zao anawashughulikia katika kipindi kifupi.

No comments:

Post a Comment

Pages