HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 28, 2020

Idriss Sultani aachiwa huru, akamatwa tena

Na Janeth Jovin


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru Msanii wa Vichekesho, Idriss Sultan (27) na wenzake wawili na kisha kukamatwa tena na kusomewa upya mashtaka ya kuchapisha maudhui bila leseni ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Mbali na Sultan ambaye ni Mkazi wa Mbezi Beach  jijini Dar es Salaam, washtakiwa wengine ni Dokta Ulimwengu (28) Mkazi wa Msasani na Isihaka Mwinyimvua (22) Msanii na Mkazi wa Gongo la Mboto.

Mapema leo Julai 28,2020 washtakiwa hao walifika mahakamani hapo kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali kufuatia upelelezi kukamilika kitambo lakini upande wa mashtaka ulidai bado hawajakamilisha kuandaa maelezo hayo hivyo wanaomba kesi iahirishwe.

Hata hivyo baada ya taarifa hiyo kutoka upande wa mashtaka Hakimu Mkazi Mkuu Hurum Shaidi aliifuta kesi hiyo na washitakiwa walikamatwa na kusomewa upya mashitaka hayo.

Akiwasomea mashtaka mapya wakili wa Serikali, Adolf Ulaya amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga kuwa washitakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Machi 8,2016 na Machi 12,2020 maeneo ya jiji la Dar es Salaam.

Amedai siku hiyo, washtakiwa hao walichapisha maudhui kupitia chaneli ya Local Motion ya YouTube bila kuwa na leseni ya TCRA.

Washtakiwa wamekana  kutenda makosa hayo wako nje kwa dhamana baada ya kufanikisha kutimiza masharti ya dhamana yaliyowataka kila mmoja kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya sh. Milioni tano kila mmoja.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kesi imeahirishwa hadi Agosti 8, mwaka huu kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.

No comments:

Post a Comment

Pages