Muonekano wa ujenzi wa Daraja la Mto Mjonga (suspension foot bridge),
liliopo Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro, linalojengwa na Wakala wa
Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), likiwa limefikia asilimia 80
kukamilika, daraja hili ni kiunganishi cha Vijiji vya Digoma na
Digalama.
NA ERICK MWANAKULYA, MOROGORO
WAKAZI
wa Kijiji cha Digoma, kata ya Diongoya Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero
Mkoani Morogoro wameipongeza Serikali kupitia Wakala wa Barabara za
Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kujenga daraja la kudumu katika mto
Mjonga litakalounganisha Kijiji hicho na maeneo mengine ya Wilaya ya
Mvomero.
Wakizungumza
katika mahojiano maalum wakazi hao wameipongeza TARURA kwa kujenga
daraja hilo litakalotumiwa na watembea kwa miguu pia litapitisha na
baadhi ya vyombo vya usafiri kama pikipiki na bajaji.
“Kivuko
kikikamilika kitatuondolea kero ya muda mrefu kwani maji yanapojaa
tunapata shida sana kupata huduma za kijamii hivyo kukamilika kwa daraja
hili kutapunguza kero zetu za muda mrefu”, alisema Leonard Michael
Mkazi wa Kata ya Diongoya.
Wakazi
hao wamesema kuwa kwa sasa wanatumia shilingi 1000 hadi 2000 kuvuka
kwenda upande mwingine kwa kutumia mtumbwi, hivyo kukamilika kwa daraja
hilo kutawasaidia sana katika usafirishaji wa mazao yao kwenda sokoni.
Naye,
Mtendaji wa Kijiji cha Digoma, Ndg. Omari Nyilika alisema kuwa Daraja
la Mto Mjonga ni kiunganishi cha Vijiji vya Digoma na Digalama, hivyo
ukamilikaji wa daraja hilo utawasaidia wakazi hao katika shughuli zao za
kijamii na kuboresha uchumi wao kwani wanategemea zao la Hiliki pamoja
na Kokoa.
“Tunaishukuru
sana TARURA kwa kutujengea daraja hili kwani Kijiji chetu hakikuwa na
mawasiliano kwa muda mrefu kiasi kilichopelekea wananchi kupata shida
kuvuka kwenda upande wa pili kufanya shughuli zao za kimaendeleo, lakini
kwa jitihada za TARURA kivuko cha kudumu kimejengwa ili kutatua kero
hiyo ya muda mrefu’’, alisema Mtendaji huyo.
Naye,
Meneja wa TARURA Halmashauri Wilaya ya Mvomero, Mhandisi William Lameck
alisema ujenzi wa Daraja hilo umekuja baada ya mawasiliano kukatika
hasa kipindi cha masika na kusababisha shughuli za maendeleo kukwama na
kushindwa kufanya kazi zao kwa kuwa wakazi wa Kata ya Diongoya uchumi
wao mkubwa unategemea mazao ya kokoa pamoja na hiliki ili kujipatia
kipato.
Ujenzi wa daraja
la Mto Mjonga lenye urefu wa mita 42 umefikia asilimia 80 kukamilika na
utagharimu shilingi milioni 68.1, ambapo kukamilika kwake kutawezesha
wananchi kuvuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine ikiwa ni pamoja na
kufikisha mazao yao sokoni kwa urahisi.
No comments:
Post a Comment