HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 09, 2020

BORESHENI HUDUMA ZA JAMII KUPUNGUZA GHARAMA ZA MATIBABU: NAIBU WAZIRI DKT. MOLLE

 

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel amesema iwapo Serikali na wananchi watashirikiana pamoja katika kuitumia vyema Kada ya Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii itapunguza gharama za matibabu na mahitaji ya huduma za Afya kwa wananchi.

Dkt. Mollel amesema hayo alipotembelea Banda la Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii katika maonesho ya Nanenane kwenye Viwanja vya Nyakabindi Bariadi, Mkoani Simiyu.

Amesema kuwa katika kuimarisha huduma zinazotolewa na Idara ya Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii wananchi na Serikali katika ngazi za Wilaya na Kata wanapaswa kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha Wataalam wa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii wanasaidia wananchi kuondokana na changamoto zinazowakabili.

Ameongeza kuwa Wataalam wa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii wamesaidia matatizo mengi ya kijamii kutapatiwa ufumbuzi hivyo kupunguza gharama zisizokuwa za lazima hasa katika kuzuia kwa kusambaa kwa magonjwa yanayozuilika.

Aidha, Dkt. Mollel ameipongeza Wizara kwa jitihada zinazoendelea kupitia elimu kwa umma sambamba na utoaji wa ushauri na unasihi kwa Wananchi wanaotembelea Banda la Wizara hiyo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Afya Profesa Mabula Mchembe amehimiza msisitizo utolewe katika uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) ili huduma zinazotolewa kwa jamii ziendane na thamani halisi ya fedha.

Amesema kuwa  baadhi ya NGOs nchini zinajikita katika huduma za kufanana na wakati mwingine katika eneo moja kwa kuacha baadhi ya maeneo kukosa huduma hizo muhimu kwa maendeleo.


Profesa Mchembe amehimiza kutolewa kwa elimu zaidi kwa umma ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ili kupata ufumbuzi wa uhakika utakaosaidia kutatua changamoto hizo.

Ameongeza kuwa Maendeleo ni pamoja na kuwashauri na kuwawezesha wananchi kutambua fursa zinazowazunguka na namna ya kuzitumia ili kujikwamua kiuchumi na kuchangia kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Pages