Na Janeth Jovin
Mkazi wa Manzese Argentina jijini Dar es Salaam, Asha Juma amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabili na mashtaka mawili ya kumiliki risasi 45 kinyume cha Sheria.
Asha alifikishwa Mahakamani hapo leo na kusomewa mashtaka yake na Wakili wa Serikali Adolph Lema mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Agustina Mbando.
Katika shtaka la Kwanza Lema amedai mshtakiwa huyo anakabiliwa na kosa la kumiliki risasi kinyume cha sheria ambapo ilidaiwa kuwa Mei 17, 2020 katika eneo la Manzese jijini Dar es Salaam alikutwa akimiliki risasi 29 zenye kipenyo milimita 12 kinyume cha sheria ya usimamizi wa silaha na risasi.
Katika shtaka la pili Asha anadaiwa kumiliki risasi kinyume cha sheria kosa ambalo linadaiwa kuwa amelitenda Mei 17, 2020 katika eneo la Manzese jijini Dar es Salaam, ilidaiwa kuwa alikutwa akimiliki risasi 16 zenye kipenyo cha milimita 9 kinyume na sheria ya usimamizi wa silaha na risasi.
Wakili Lema alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo aliomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina Mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hivyo amerudishwa rumande kwa kuwa mashtaka yanayomkabili hayana dhamana. Kesi imeahirishwa hadi Agosti 26, 2020
No comments:
Post a Comment