VICTOR MASANGU, RUFIJI
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo ametoa muda wa siku saba kukamatwa kwa mfugaji mmoja kwa tuhuma za kutenda kosa la kumbaka bibi mmoja anayekadiriwa kuwa na zaidi ya miaka 60 akiwa shambani kwake nyakati za usiku kwa ajili ya kulinda mazao yake yasiliwe na mifugo na kumsababishia maumivu makali kwa kile kinachodaiwa ni kuwepo kwa migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Ndikilo ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara na baaadhi ya wananchi wa kata ya Mkongo iliyopo Wilayani Rufiji ikiwa ni katika mwendelezo wake wa ziara ya kikazi yenye lengo la kutembelea miradi mbali mbali ya maendeleo pamoja na kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili wananchi ili kuweza kuzifanyia kazi ambapo ameambatana na kamati ya ulinzi na uslama ya Mkoa.
“Mkuu wa Polisi hiki kitendo alichofanyiwa huyu mama ni kitendo cha kinyama sana na mimi naagiza kwamba natoa muda wa siku saba tu yani wiki moja huyo mtuhumiwa ambaye amefanya kitendo cha kubaka akamatwe mara moja ili sheria iweze kufuata mkondo wake kwani haiwezekani mambo kama haya yafanyanyika na jeshi la polisi lipo tuu hakamatwe mara moja,”alisema Ndikilo.
Aidha Ndikilo alisema kwamba serikali yake ya Mkoa wa Pwani kamwe haiwezi kufumbia macho mambo kama hayo kwa wananchi kufanyiwa vitendo vya kikatili na kwmaba wale wote ambao watabainika kuhusika katika matukio mbali mbali kama hayo watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria ili iwe fundishi kwa wengine.
Katika hatua nyingine Ndikilo amewataka watendaji wa vijiji pamoja na wenyeviti wa vijiji ambao watakuwa wazembe katika kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji kwa kipindi cha mwezi mmoja endapo akiona bado kunaendelea migogoro ya ardhi ameahidi kuwashughulikia mara moja na kuwataka wajiondoe kabisa katika nafai hizo ili wachaguliwa viongozi wengine ambao wanawajali wananchi.
Kwa upande wake Bibi huyo aliyejulikana kwa jina la Tatu Lupamba ambaye alifanyiwa kitendo hicho cha ukatili wa kubakwa ametoa kilio chake Kwa Mkuu wa Mkoa ambapo amedai kuwa alifanyiwa kitendo hicho mwezi wa sita mwaka huu wakati akiwa shambani kwake na mfugaji mmoja ambaye hakuweza kumfahamu kwa sura na kuiomba serikali kuingilia kati sakata hilo.
Akizungumzia kuhusu tukio hilo la ubakaji Mkuu wa Polisi kituo cha Polisi Wilaya ya Rufiji Wilbert Siwa amekiri mbele ya wananchi kuwa ni kweli taarifa hizo limesharipotiwa na kwamba tayari wameshafungua jalada na kwamba wanaendelea na uchunguzi ili kuweza kumbaini muhusika ili aweze kuchukulia hatua za kisheria .
“Ni kweli tukio hili Mkuu wa Mkoa la mama huyo tulilipata na kwamba tumeshaanza kulishughulikia na lilitokea tarehe 28 ya mwezi wa sita ambapo mama huyo alikukuja kutoa malalamiko yake ya kwamba amebakwa na mtu mmoja ambaye ni mfugaji wa jamii ya kisukuma na sisi tumelichukua na bado tunaendele na upelelezi kwa kuwa mtu anayetuhumiwa ajajuliakana,”alisema Siwa.
Pia katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Polisi alisema kwamba wataendelea kuimarisha ulinzi kwa wananchi katika maeneo mbali mbali ya Wilaya ya Rufiji na kwamba lengo lao kubwa ni kuhakikisha wanadumisha hali ya ulinzi na usalama na kwamba mtuhumiwa aliyefanya kosa hilo bado anaendelea kutafutwa.
Wilaya ya Rufiji iliyopo Mkoa wa Pwani katika baadhi ya maeneo yake bado yanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuwepo kwa migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo kwa kiasi kikubwa inasababishwa na wenyeviti wa vijiji na vitongoji hali ambayo wakati mwingine inapelekea kuwepo kwa mapigano ambayo yanasababisha hali ya uvunijfu wa amani.
No comments:
Post a Comment