HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 16, 2020

Mvomero wakaribisha wadau USMJ

Ofisa Misitu wa Wilaya ya Mvomero, Edward Kimweri akifafanua jambo kwa waandishi wa habari pichani hawapo, kuhusu Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ), ilivyo na mchango kwenye uhufadhi wa misitu na mazingira wilayani hao kulia ni Mkurugenzi wa Halmashsuri ya Mvomero Hassani Njama.
Ofisa Sera na Majadiliano wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA), Elida Fundi akimkabidhi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mvomero machapisho mbalimbali kuhusu dhana nzima kuhusu Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ).
 

Na Suleiman Msuya


HALMASHAURI ya Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro, imewakatibusha wadau mbalimbali wa uhifadhi wa mazingira na misitu ili waweze kushirikiana pamoja kutoa elimu ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ).

Ukaribisho huo umetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Hassani Njama wakati akizungumza na waandishi wa habari waliomtembelea hivi karibuni ili kujua namna halmashauri yake inasimamia dhana ya USMJ.

Njama alisema Mvomero ni moja ya wilaya ambayo bado ina changamoto za uhifadhi hivyo anaamini iwapo wadau wengine watajitokeza na kushiriana na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Jamii Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) changamoto hiyo itaisha.

"Nitumie nafasi hii kuwakaribisha wadau wa kama TFCG na MJUMITA ambao kupitia mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswis (SDC), wameweza kutusaidi USMJ ambayo ilikuwa hati hati kupotea.

Tuna vijiji 10 hivyo lengo letu ni Kuongeza vijiji vingine vipya kwani manufaa yapo ni imani yangu kuwa katika bajeti ya 2020/2021 tunaweza kuanza," alisema.

Njama alisema mkakati wao mkubwa pamoja na kuomba wadau wengine watahakikisha wanatoa elimu kwa wanavijiji ambao wanamiliki misitu ya vijiji pamoja na viongozi ili kila mmoja awe balozi wa USMJ.

Alisema USMJ katika wilaya yao itatekelezeka kwa urahisi kutokana na vijiji 101 kati 167 kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi.

Aidha, Njama alitoa rai wa taasisi na mashirika ambayo yanajihusisha na mpango wa matumizi bora ya ardhi kusimamia mchakato huo hadi ufike mwisho ili jamii inufaike.

Ofisa Misitu wilaya ya Mvomero Edward Kimweri alisema mradi wa TTCS umechochea maendeleo na uhifadhi kwa kiwango kikubwa hivyo wao wataendelea kuungana na wadau wengine ambao wanahitaji kushirikiana.

Alisema jamii ambayo ina misitu ya asili na ile ya Serikali kuu imekuwa mwalimu mzuri katika kulinda na sababu kubwa ni kutokana na manufaa ambayo wanayaona.

"Kusema ukweli mradi huu wa TTCS umeturahisishia kazi sana sisi watumishi wa sekta ya misitu kwani tumekuwa na mabalozi wengi pale ambapo hali ya uharibifu inatokea naungana na ombi la mkurugenzi kuwakaribisha wadau wengine," alisema.

Alisema vijiji ambayo vipo kwenye mradi vimekuwa na mipango mingi ya maendeleo jambo ambalo tunataka kulisambaza kwa vijiji vingine.

Aidha, akizungumzia tangazo la Serikali GN 417 Ofisa Misitu huyo alisema kwa mtazamo wake anaona ina faida na hasara hivyo kinachotakiwa ni watu wote wajipange kukabiliana nayo kwa maslahi ya misitu.

Kwa upande wake Ofisa Sera na Majadiliono kutoka MJUMITA, Elida Fundi alimueleza sababu ya wao kujikita katika USMJ ni kuhakikisha rasilimali misitu na mazingira yanakuwa salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Alisema mradi wa TTCS umefikia kikomo Novemba 2019 lakini wamekuja na mradi mwingine ambao utajikita katika mafunzo kwa ngazi zote.

"Kwa takribani miaka nane tumekuwa tukitekeleza mradi wa TTCS, ila kwa sasa tumekuja na Mradi wa Kuhifadhi, Misitu kwa Kuwezesha Biashara Endelevu ya Mazao ya Misitu Tanzania (CoForEST) ni imani yangu tutaenda pamoja ili misitu yetu iwe salama na endelevu," alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages