Na Bryceson Mathias, Arusha
MKUU wa Mkoa wa Arusha, Idd Hassan Kimanta, ametoa Salamu za rambirambi kufuatia vifo vya wanafunzi watatu kati ya watano waliogongwa na gari katika ajali ilioyotokea jioni ya tarehe 06/08/2020 eneo la Kisongo.
Katika taarifa hiyo kwa umma, Kimanta amewapa pole Wazazi, Waalezi na Wanancho wote wa Mkoa wa Arusha kwa msiba uliotokea mapema jana jioni ambapo wanafunzi watano waliokuwa wakitoka shuleni waligongwa na gari na watatu kufariki huku wawili wakijeruhiwa.
Taarifa hiyo kwa umma iliyotolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha ilisema, Wanafunzi watano waligongwa na gari wakiwa wanatoka shuleni ilisema, wanafunzi watatu kati ya watano walipoteza maisha na wawili walijeruhiwa.
Aidha iliainisha kwamba waliokufa ni pamoja na wasichana wawili na mvulana mmoja ambapo majina yao, Shule wanayosoma pamoja na gari lililowagonga taarifa yake itatolewa baadaye kutokana na kusubiri hatua za uchunguzi na utambulisho toka vyombo husika vikiwemo vya ulinzi na usalama.
Hata hivyo imenukuliwa kwamba, Majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Maunt Meru mkoani humo na taarifa kamili zinatarajiwa kupatikana mara baada ya uchunguzi wa kina wa Kitabibu utakapokamilika.
Wakati huo huo Wananchi waliohojiwa kwa nyakati tofauti katika eneo la tukio wamesikitishwa na tukio hili na kudai kwamba, Madereva hawako makini na watembea mbarabarani na hasa kwenye maeneo ambayo wanafunzi wanapita au kukatisha barabara.
Wameilalamikia serikali kwamba, barabara nyingi hapo mkoani alama nyingi zimekuwa hazionekani vizuri na kama zipo basi madereva wamekuwa hawazizingatii na kuzitii na matokeo yake wanaendesha kama wanavotaka kwa kushindana kutaka kuwahi na matokeo yake ni kupoteza viongozi wa kesho kwa ajali kama hizo.
Wamependekeza Askari wa Barabarani kuwepo kwenye maeneo ya wanapopita wanafunzi ili kuwasaidia kupita kwa kuyasimamisha magari,, lakini bila hivyo madereva wanawadharau wanafunzi.
No comments:
Post a Comment