Na Janeth Jovin
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imesema kuwa itaingia mkataba wa makubaliano (MOU) na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), utakaokuwa na lengo la kuwafundisha wafanyakazi wa bandari ili waongeza ufanisi na kuendana na kasi ya upanuzi wa bandari hiyo.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Elihuruma Lema kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, wakati wa ziara ya Baraza la Uongozi wa NIT, likiongozwa na Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Zacharia Mganilwa.
Lema amesema wameona NIT wameingiza mawazo ya TPA katika mitaala yao ambayo ni jinsi ya kuwafundisha wafanyakazi wa bandari kuendesha mitambo jambo ambalo wanalihitaji kufanyika kwa watumishi wao.
"Kutokana na mitaala hiyo sasa tunatarajia kufanya nao kazi NIT hasa kwa kuingia nao MOU ya kuangalia ni jinsi gani tutakuwa tunawapa mafunzo wafanyakazi wetu ili kuongeza ufanisi wa bandari na kuendana na kazi ya upanuzi wa kina cha bahari ambao unaendelea kufanyika hivi sasa," amesema Lema.
Hata hivyo Lema amesema ujio wa Baraza la uongozi la chuo hicho bandarini hapo unatarajiwa kufanikisha mengi katika kuendelea kuboresha bandari, ambapo kwa sasa wameanzisha programu mbali mbali ambazo wanatarajia kuanza kuzitoa.
Naye Mkuu wa chuo hicho, Profesa Mganilwa amesema kwa sasa NIT ina mitaala mipya miwili ambayo itaanza kufundishwa mwaka huu ambayo inalenga kupata wataalamu wa usafirishaji kwa njia ya barabara na reli na wataalamu wa oparesheni za bandari na mashine za meli kubwa.
Amesema kabla ya kuanza kwa mitaala hiyo waliwashirikisha TPA ili wakianza kutoa kozi ziendane na mahitaji ya mamlaka hiyo na malengo ya Serikali ya awamu ya tano ya kufikia uchumi wa viwanda .
"Tumeshaikamilisha ile mitaala na kuja kwetu hapa baada tulikuwa na lengo la kuwaeleza kwamba mawazo yenu yote TPA mliyoyatoa tumeyaingiza kwenye mitaala yetu mipya, kuanzia Novemba tutaanza kudahili wanafunzi wapya wanaohusiana na upanuzi wa bandari," amesema Profesa Mganilwa na kuongeza
"Kama mlivyomsikia Mkurugenzi alisema asilimia 50 ya wafanyakazi wa TPA ni wanafunzi wetu, kwa hiyo nahitaji yao yataongezeka ndiyo maana tumekuja na bodi ili wajue wanafunzi baada ya kumaliza wanakwenda wapi," amesema
Mkurugenzi huyo, amesema lazima changamoto za TPA wazichukue wazibadilishe ziwe fursa, mfano, upanuzi wa bandari unaenda na malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano, kwa hiyo kutahitajika wataam kuendana na kasi ya uchumi wa viwanda.
Naye, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Mhandisi, Profesa Bavo Nyichomba aliiomba TPA itoe nafasi kwa wanafunzi wa NIT kufanya mafunzo kwa vitendo kabla hawajaanza kufanya kazi.
"Tunaomba wanafunzi kabla ya kumaliza kozi zao waje wachukue mafunzo ya vitendo katika nyanja tofauti ili wakimaliza wachukue muda mfupi kwenda kwenye mafunzo mengine kabla ya kuanza kazi,"
"Hii itatusaidia kuondokana na mafunzo ya wiki tatu, tatu ambapo mwanafunzi anamaliza akiwa hana kitu, tufike mahali tuweke programu, ambayo mwanafunzi akifika mwaka watatu anaachia anakuja huku anafanya mafunzo ya mwaka mmoja halafu anarudi shule kumaliza, "amesema Profesa Nyichomba
No comments:
Post a Comment