HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 13, 2020

VIJANA WALIOKOPA MIKOPO YA HALMASHAURI WATAKIWA KUIREJESHA

 

Na Janeth Jovin

HALMASHAURI  ya Manispaa ya Ilala imewataka vijana kuhakikisha wanarudisha mikopo yote waliyokopeshwa na halmashauri hiyo kwenye vikundi vyao ili kuweza kutoa fursa ya vikundi vingine kukopeshwa.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam jana na Ofisa wa Vijana Manispaa hiyo, Sapiencia Masaga wakati wa mkutano wa viongozi wa serikali na wadau wengine ulioandaliwa na Shirika lisilo la Serikali la CAFLO chini ya ufadhili wa Shirika la Foundation for Civil Society kwa lengo la kutengeneza mikakati ya kutatua changamoto zinazowakabili vijana kiuchumi.

Masaga ametoa kauli hiyo baada ya viongozi wa Mtandao wa Majukwaa ya Vijana (Mtamavita) kutoka Buguruni, Vingunguti, Kipawa, Mnyamani na Tabata kulalamika katika mkutano huo kuwa kuna vikundi vina zaidi ya miezi sita na mwaka bado havijapatiwa mikopo.

Akijibu swali hilo, Masaga alisema vikundi vingi vya vijana katika halmashauri hiyo havirejeshi mikopo waliyokopeshwa  jambo ambalo linalokwamisha vikundi vingine kushindwa kukopeshwa fedha na kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

“Vikundi vya vijana kiukweli mnatutesa maana amrejeshi mikopo yenu jambo hili linatukwamisha katika kuwahudumia vijana wengine, niwaambie mkiendelea hivyo upo mpango unaotaka msikopeshwe kabisa sasa ili suala hilo lisitokee hakikisheni mnarejesha kwa haraka na wakati mliopangiwa.

“Mpaka sasa tuna vikundi zaidi ya 3000 ambavyo vimeomba mikopo na fedha zilizotengwa kwa mwaka huu wa fedha kiasi cha Sh.Bilioni 4.9 zimetengwa kwa ajili ya kukopesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu hivyo tunachokifanya tutaangalie yale makundi yaliyokuwa yakifanya vizuri katika urejeshwaji wa fedha,” amesema

Aidha Magasa amevishauri vikundi vingine vya vijana kuomba mikopo katika Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam kwani na wao wanatoa mikopo hiyo.

“Jiji sasa hivi hawana watu wa kukopa na walishakuja kwetu kutuambia basi niwaombe vijana muende huko mkikutana na masharti hakikisheni mnayatekeleza na sio mnakata tama,” alisema Masaga

Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya majukwaa ya vijana yaliyoundwa katika mitaa na kata za Vingunguti, Kipawa, Mnyamanj, Buguruni na Tabata, Katibu wa Mtawanita, Shaban Mbwembwe alisema  jumla ya majukwaa 37 ya vijana yameundwa katika kata hizo.

Alisema mafanikio yaliyopatikana ni jumla ya majukwaa 15 kati ya hayo 37 yamesajiliwa katika ngazi ya Manispaa ya Ilala na kuongeza kuwa majukwaa sita kati ya hayo 15 yameshapatiwa mikopo.

"Baadhi ya vijana waliopo kwenye majukwaa wamepata mafunzo ya ujasiriamali kwa vitendo na wanaendelea kufanya shughuli zao zinazowaongezea kipato," alisema

Hata hivyo Mbwembwe alisema pamoja na mafanikio hayo bado wanakabiliwa na changamoto ya vipindi hivyo kucheleweshewa mikopo waliiomba halmashauri.

"Kuchelewa kupata kwa mikopo hiyo kunasababisha vijana wengi kushindwa kutekeleza miradi yao katika muda waliopanga," alisema

Aidha Mratibu wa Miradi ya CAFLO, Emmanuel Ngazi alisema shirika hilo chini ya ufadhili wa Shirika la Foundation for Civil Society wamekuwa wakitoa mafunzo ya vitendo kwa vijana wajasiriamali  yanayolenga kuwawezesha vijana kujitegemea kimaisha kwa kufanya ujasiriamali utakaowapatia kipato.

Naye Ofisa Maendeleo Kata ya Mnyamani, Upendo Ngailo alisema wataendelea kuwasimamia vijana kupata mikopo ili kuendelea mitaji na biadhara zao za kila siku.

No comments:

Post a Comment

Pages