HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 19, 2020

Benki ya CRDB yapewa ubalozi wa mazingira

Na Mwandishi Wetu

BENKI ya CRDB imeteuliwa kuwa balozi wa mazingira wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Pendezesha Tanzania iliofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Goba, iliyopo Dar es Salaam jana.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mussa Azza ‘Zungu’ aliiteua benki hiyo alipokuwa akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge.

Waziri Zungu aliipongeza Benki ya CRDB kwa utekelezaji wa mikakati ya kusaidia jitihada za Serikali katika kutunza na kuboresha mazingira kupitia kampeni ya Pendezesha Tanzania inayohamasisha umuhimu wa upandaji miti na kutunza mazingira.
 
Alisema kampeni ya Pendezesha Tanzania imekuja wakati muafaka kwani inaenda sambamba na mkakati wa serikali wa kupanda miti milioni 1.5 kila Halmashauri kwa mwaka ili kutekeleza Mpango wa Kitaifa wa Kupambana na Kuenea kwa hali ya Jangwa na Ukame.  
 
“Niipongeze Benki ya CRDB kwa ubunifu huu mliokuja nao wa kuwahamasisha watanzania kutunza mazingira yaliyowazunguuka.

“...Niwaahidi tu kwamba Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi hizi ili kwa pamoja tufikie lengo la kuboresha na kuyatunza mazingira yetu kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema Waziri Zungu huku akizitaka taasisi nyingine kuiga mfano Benki ya CRDB katika kuweka kipaumbele suala la utunzaji wa mazingira.
 
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kunenge aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuzindua kampeni ya Pendezesha Tanzania katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Kunenge aliwataka wananchi wa mkoa huo kupanda mti mmoja kila mtu katika makazi yake kama sehemu ya kutekeleza kampeni hiyo.

“Asanteni sana Benki ya CRDB kwa kutupa heshima wakazi wa Dar es Salaam ya kutupendezeshea jiji letu. Niwaahidi kuwa tutashiriki kikamilifu kuhakikisha tunafikia malengo,” alisisitiza Kunenge.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema kampeni hiyo ni muendelezo wa utekelezaji wa sera ya benki hiyo kusaidia shughuli za maendeleo katika jamii ambayo inaelekeza asilimia moja ya faida kila mwaka kusaidia sekta za elimu, afya na utunzaji wa mazingira.
 
“Lengo la kuzindua kampeni hii ni kuendelea kuihamasisha jamii kuona jukumu la kupanda miti ni la jamii nzima. Tumeanza kwa kupanda miti 2,000 katika shule zote za msingi na sekondari zilizopo katika Kata ya Goba kwa lengo la kuzifanya shule hizi kuwa na mazingira bora na rafiki kwa watoto kusoma,” alisema Nsekela.
 
Kampeni ya Pendezesha Tanzania inatarajiwa kufanyika nchi nzima ili kuwajengea watanzania utamaduni wa kupanda na kutunza miti katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

“Tumeanzia Dar es Salaam lakini lengo letu ni kufika katika wilaya na vijiji vyote Tanzania nzima,” aliongezea Nsekela.
 
Sambamba na uzinduzi wa kampeni ya Pendezesha Tanzania, Benki ya CRDB pia imetoa msaada wa pampu za maji kwa shule za Sekondari za Fahari, Goba na Kinzudi ili kurahisisha upatikanaji wa maji kwenye shule hizo.
 
Akizungumza juu mikakati ya biashara inayozingatia mazingira, Nsekela alisema Benki ya CRDB imejiwekea mfumo wa biashara ambao unazingatia utunzaji wa mazingira ikiwamo kuweka sera inayoelekeza utoaji wa mikopo kwa miradi inayozingatia utunzaji wa mazingira, kuanzisha huduma na bidhaa za kidijitali na kuwekeza katika mifumo ya ufanyaji kazi inayopunguza matumizi ya karatasi.
 
Ofisa Elimu Kata ya Goba, Edward Shilamba aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuanzisha kampeni hiyo ya upandaji miti katika shule za Sekondari na Msingi za kata ya Goba.

Alimhakikishia Waziri Zungu kuwa wataweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha miti hiyo inastawi kama inavyotarajiwa.
 
Kutokana na jitihada za kusaidia utunzaji mazingira mpaka, mwaka jana Benki ya CRDB ilikuwa benki ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kutambuliwa na kupata usahili katika Mfuko wa Umoja wa Mataifa unaoshugulikia masuala ya Tabia Nchi “United Nations Green Climate Fund (GCF)”.

Kupitia usahili huu, Benki ya CRDB sasa inaweza kushiriki katika kuwezesha miradi mikubwa ambayo ni rafiki wa mazingira, kwa kutoa mikopo ya hadi dola za kimarekani milioni 250 kwa mradi mmoja.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mussa Azan Zungu akipanda mti wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Pendezesha Tanzania iliyozinduliwa kwa ushirikiano baina ya Benki ya CRDB na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira. Uzinduzi wa kampeni hiyo ambayo ina hamasisha upandaji miti ilizinduliwa katika shule ya Sekondari Goba, Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mussa Azan Zungu (watano kushoto) akiwa katika picha ya pomoja na Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge (wanne kushoto), Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori (watano kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (katikati) na viongozi wengine wa Serikali na Benki ya CRDB wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Pendezesha Tanzania. Viongozi hao walishikana mikono kuonyesha ishara ya ushirikiano katika kutimiza malengo ya kupanda miti milioni 1.5 kila wilaya kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali katika utunzaji mazingira.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Ndugu Abdulmajid Mussa Nsekela,akipanda mti katika viwanja vya shule ya Sekondari Goba,jijini Dar es Salaam leo Septemba 19, 2020, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Pendezesha Tanzania.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge, akipanda mti katika viwanja vya shule ya Sekondari Goba, jijini Dar es Salaam leo Septemba 19, 2020, kwenye Uzinduzi wa kampeni ya Pendezesha Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Pages