Maombi 92,947 yapokelewa
na kusajiliwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Abdul- Razaq Badru (katikati) akizungumza na waandishi wa vyombo vya habari Agosti 31 mwaka huu kuhusu kuongezwa kwa muda katika dirisha la maombi ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu katika mwaka wa masomo 2020/21. Kushoto ni Meneja Masoko wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Joseph Kimaro na kulia ni Meneja Mkuu Uendeshaji Biashara wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) Mwanaisha Said. (PICHA NA BODI YA MIKOPO- HESLB).
Na Mwandishi Wetu, HESLB, DAR ES SALAAM
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza kufungwa kwa dirisha la maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao kwa mwaka wa masomo 2020 ambapo hadi kufikia leo Septemba 10, 2020 imepokea na kusajili jumla ya maombi ya wanafunzi 92,947.
Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi (Septemba 10, 2020) Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa (HESLB), Abdul-Razaq Badru imesema mfumo wa maombi hautaweza kuruhusu usajili wa maombi mapya ya waombaji isipokuwa kwa waombaji 7,500 waliopo mtandaoni ambao hawajakamilisha maombi hayo.
Badru amesema HESLB ilifungua dirisha la maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao kwa muda wa siku 40 kuanzia tarehe 21 Julai mwaka huu, ambapo hata hivyo kufuatia maoni na maombi ya wazazi, walezi na wanafunzi iliongeza muda wa siku 10 hadi leo Alhamisi Septemba 10, 2020 ili kutoa fursa kwa waombaji kukamilisha maombi hayo.
“Leo Alhamisi (Septemba 10, 2020) saa 6:00 usiku dirisha la upokeaji wa maombi ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2020/2021 kwa njia ya mtandao, litafungwa rasmi. Baada ya muda huo, usajili mpya kwa ajili ya maombi mapya hautaruhusiwa’’ alisema Badru
AIdha, Badru alisema Oktoba Mosi mwaka huu HESLB itaanza zoezi la uchambuzi wa maombi hayo na baadaye itaorodhesha maombi yote yenye mapungufu na kuwatangazia waombaji husika kwa ajili ya kurekebisha kasoro zilizojitokeza.
Akifafanua zaidi, Badru aliwataka wazazi, walezi na wanafunzi kuendelea kufuatilia vyanzo rasmi ikiwemo tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz) kuhusu taarifa muhimu na orodha ya watakaopangiwa mikopo kwa mwaka wa masomo 2020/2021 kwa mujibu wa kalenda ya mwaka wa kitaaluma (academic almanac) ya mwaka huu.
No comments:
Post a Comment