NA MWANDISHI WETU
Serikali
za Tanzania na Ufaransa zimeingia makubaliano ya kutoa mafunzo ya mbinu
za kufundishia lugha ya Kifaransa kwa walimu 100 nchini ambao watakuwa
na uwezo wa kufundisha wanafunzi 5,000 wa Kitanzania katika ngazi ya
sekondari.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao kati ya
Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Frederic Clavier na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Elimu, Sayansi Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo
kilichofanyika Jijini Dar es Salaam ambapo jumla ya Dola za Kimarekani
250,000 zitatumika ili kufanikisha mpango huo.
Katika kikao hicho
wamekubaliana kufanyika kwa vikao vya kitaalamu kati ya Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia na Kituo cha Ubalozi wa Ufaransa (Alliance
Francais) ili kupanga utekelezaji wa mafunzo haya ya walimu.
Aidha,
Balozi Clavier ameonesha ameeleza uwepo wa fursa za Watanzania kusoma
programu zisizopungua 2,000 za Kiingereza nchini Ufaransa. Ameelezea
kuwa Ufaransa inaandaa Maonesho ya Elimu ya Juu (Higher Education Fair)
yatakayofanyika nchini Mei 2021 ambapo vyuo 20 vya Ufaransa
vitashiriki kutafuta ushirikiano na Vyuo Vikuu vya Tanzania na Sekta
binafsi.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu Akwilapo
ameushukuru Ubalozi wa Ufaransa kwa kuendeleza ushirikiano katika kukuza
na kuimarisha elimu ya Juu nchini kupitia ufadhili wa masomo hayo na
kuagiza wahusika katika Wizara anayoisimamia kuhakikisha vikao vya
kitaaluma vinafanyika ili mafunzo hayo yaweze kuanza kwa wakati
uliopangwa.
Katibu Mkuu Akwilapo pia ameahidi kuweka wazi kwa
Watanzania kuhusu uwepo wa fursa hizo za kusoma programu za Kiingereza
nchini Ufaransa ili Watanzania waweze kuchangamkia fursa hiyo.
No comments:
Post a Comment