NA JANETH JOVIN
MFANYABIASHARA maarufu jijni Tanga, Yanga Omary Yanga, ambaye anafahamika kwa jina maarufu la “Rais wa Tanga” amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya aina na herion zenye uzito wa gramu 1052.63.
Hukumu hiyo imetolewa leo na Mahakama Kuu, Kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi mkoani Tanga.
Hata hivyo, Mahakama hiyo imewaachia huru washtakiwa wengine katika kesi hiyo ambao ni Rahma Juma, ambaye ni mke wa mfanyabiashara huyo na Halima Mohamed, ambaye ni mfanyakazi wa ndani, kwa ushahidi hafifu uliotolewa dhidi yao.
Jaji Imakulata Banzi aliyekuwa anasikiliza shauri hilo katika Mahakama Kuu, Kanda ya Tanga, alifikia uamuzi huo leo mara baada ya kumtia hatiani mfanyabiashara huyo kwa kosa lililokuwa linamkabiri kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.
Amesema kuwa upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Faraja Nchimbi umeweza kupitia mashahidi saba na vielelezo kumi umeweza kuthibitisha bila kuacha shaka yoyote kuwa Yanga Omari alikuwa akijihusisha na biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya.
“Kwa kuzingatia ushahidi huo, mahakamahii inamtia hatiani mshitakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa z kulevya kama alivyoshitakiwa,” Jaji huyo amesema.
Mawakili wengine waliokuwa wanaiwakilisha jamhuri katika shauri hilo ni Wakili Mwandamizi Pius Hilla, Mawakili wa Serikali Constantine Kakula, Salimu Msemo, Donata Kazungu na Mseley Mfinanga, ambaye ni mwanasheria mwandamizi kutoka Mamlaka ya Kuzuia Dawa za Kulevya (DCEA).
Jaji Banzi amesema kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha shtaka hilo dhidi yao kwa vile tangu mwanzo taarifa kuhusu kutendeka kwa kosa hilo zilitolewa zikimhusisha mshitakwa wa kwanza (Yanga).
Ameeleza kuwa mshtakiwa wa pili (Rahma) hakuhusishwa kwa namna yoyote tangu mwanzo na kwamba mshtakiwa wa tatu (Halima) alikuwa mfanyakazi wa ndani na vitu vilivyokutwa kwenye chumba chake vilithibitika haviku madawa ya kulevya.
Washtakiwa katika shauri hilo walikuwa wanawakilishwa na Mawakili Majura Magafu, Nehemia Nkoko, Mohamed Kajembe, Kahoza Nicholaus na Denis Tumaini.
Kwa mujibu wa mashtaka, kosa walilokuwa wamweshitakiwa nalo lilitendeka Octoba1, 2018, maeneo ya Bombo jijini Tanga.
Kabla ya mahakama kutoa adhabu, upande wa mashitaka uliiomba mahakama kuzingatia uzito wa kosa na adhari za madawa hayo katika jamii na katika kuathiri uchumi wa nchi. Hata hivyo, upande wa utetezi uliomba adhabu nafuu itolewe kwa mshitakiwa kwa vile ni mkosaji wa kwanza na anafamilia inayomtegemea.
Mfanyabiashara maarufu jijni Tanga, Yanga Omary Yanga, ambaye anafahamika kwa jina maarufu la “Rais wa Tanga” wa kwanza aliyevaa kanzu akiwa mahakamani pamoja na washtakiwa wengine wakati wa hukumu ya kesi inayomkabili ya kusafirisha dawa za kulevya.
No comments:
Post a Comment