HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 04, 2020

Meya Mbano awapongeza wanahabari wanawake



Na Mwandishi Wetu


MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Songea, Michael Mbano ameupongeza Umoja wa Waandishi wa Habari Wanawake  (WJ) waliompa mtaji mlemavu Gonzalva Rungu (19).

Rungu ni mlemavu wa mikono na mguu alihitimu kozi ya ushonaji kwenye Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) mjini Songea wakati wa mahafali ya chuo hicho yaliyofanyika jana.

Umoja huo kupitia mwakilishi wake Joyce Joliga ulikabidhi cherehani moja yenye thamani ya Sh. 250,000 na kiasi cha Sh. 50,000 kwaajili ya kuanza shughuli ya ushonaji alizojifunza VETA.

Akikabidhi cherehani hiyo jana  akiwa na Meya Mbano wakati wa mahafali ya 35  ya VETA, Joliga alisema WJ ni sehemu ya jamii hivyo wanapoona uhitaji wanaguswa na kusaidia ili kuonesha mfano kwa wengine wenye uwezo.

Alisema hiyo si mara ya kwanza kwa wanahabari kumsaidia Rungu na kuahidi kuendelea kumsaidia mhitimu huyo na wengine wenye mahitaji.

Akizungumza baada ya kumkabidhi Rungu cherehani na fedha hizo alisema WJ imemfurahisha kwa kuonesha utu
na kuahidi kuunga mkono juhudi za WJ kwa kutoa Sh. 500,000 ili kumsaidia Rungu na mhitimu mwenzie mlemavu ambaye hana mikono wala miguu, Riziki Ndumba.

“Waandishi wa habari wamekuwa msaada kwa jamii kwa kuibua na kuandika habari za maendeleo ambapo amewataka wananchi kushirikiana nao na kupeleka watoto wenye ulemavu chuoni kwani wanayo haki ya kupata elimu na ujuzi wa mbalimbali,” alisema Mbano.

Meya huyo pia alimshukuru Rais John Magufuli kwa kumsaidia binti huyo Sh. milioni tano ambazo zimemsaidia kupata kiwanja na makazi ya kudumu.

"Niwapongeze sana waandishi wa habari wanawake mlioguswa na kujichangisha kidogo kidogo na kisha kuja na wazo la kumsaidia mdogo wenu kwa kumnunulia mashine ya kushonea nguo, mmefanya jambo kubwa na zuri, mbarikiwe sana na muendelee kuibua na kusaidia wananchi nasi tunaendelea kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), nawaunga mkono nami nitatoa Sh. 500,000 ili ziwasaidie ndugu zetu hawa wawili Gonzalva na Riziki," alisema Mbano.

Awali Mkuu wa Chuo cha VETA Songea, Gideon Ole Lairumbe aliwashukuru waandishi hao kwa kumuwezesha Rungu na Riziki kufanya kazi ya ushonaji na kujiingizia kipato.

Alisema waandishi wameonyesha moyo wa kipekee na kuwataka wasiache kwenda chuoni hapo kuandika habari mbalimbali za kuwasaidia wananchi ikiwemo kozi zinazotolewa chuoni.

Mwenyekiti wa WJ, Esther Macha alisema umoja huo upo tayari kuwasaidia wananchi wenye mahitaji katika jamii huku wakitaka wananchi wenye uwezo wa kusaidia kufanya hivyo kwenye jamii zao.

“Tunamshukuru sana mwenzetu Joyce Joliga kwa kuibua habari ya binti huyu ambaye kwa muda mrefu amekuiwa akimsaidia kununua mahitaji ya chuo na kumpa mahitaji ya malezi ya mwanae,” alisema Macha.

No comments:

Post a Comment

Pages