HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 13, 2020

MUONGOZO KUTOLEWA MATUMIZI YA VAZI LA JOHO

 Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said amesema Wizara yake itatoa muongozo maalum juu ya matumizi ya Vazi la joho katika maskuli wakati wa mahafali ili kuliwekea heshima na hadhi yake kama lilivyo awali.


Amesema vazi hilo limekuwa likivaliwa bila ya utaratibu hali inayoweza kupelekea kumfanya mtoto kutokuwa na ari ya kuendelea kusoma.

Akizungumza katika mahafali ya Skuli ya FEZA huko Kisauni Mjini Unguja amesema utaratibu wa kuvaa joho unajuilikana kuvaliwa mpaka Mwanafunzi afike chuo kikuu na sio kumaliza mandalizi, msingi au sekondari.

Aidha Mhe Simai amewataka wazazi na walezi kushirikiana  na Walimu katika kuwalea watoto wao pamoja nankuwafuatilia kwa karibu zaidi mienendo yao ili waweze kuwa watoto wema na viongozi wazuri wa baadae.

Amesema kutokana na kuwa  elimu ni muhimu katika maisha ya mwanaadamu, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuilipia elimu kwa kutoa huduma ya hiyo kwa wote kuanzia ngazi ya maandalizi msingi hadi sekondari ya lazima ili kila mtoto aweze kupata haki hiyo ya msingi bure.

Amesema pia Serikali imetoa fursa katika Skuli binafsi, ambapo amesema Wizara itaendelea kuziuunga mkono Skuli hizo na kuziwekea miongozo na utaratibu mzuri kwa lengo la kutoa Elimu bora kwa watoto.

Aidha Mhe Simai amefahamisha kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo  ya Amali Zanzibar Ina lengo la kuanzisha mashindano ya midahalo katika Skuli kwa kutoa maada mbalimbali kwa lengo la kuongeza uelewa kwa Wanafunzi katika masuala mbalimbali pamoja na kuweka ushindani wa kimasomo kati ya Skuli moja na Skuli nyengine.

Mhe Simai amewashauri Walimu kuwafanyia wanafunzi ziara za kimasomo hasa katika  sehemu mbalimbali za kihistoria ili waweze kujifunza zaidi kwa vitendo badala ya kuishia darasani pekee.


Hata hivyo Mhe Simai ameutaka uongozi Skuli ya FEZA kufikiria juu ya suala la kusomesha lugha ya kituruki kwa wabafunzi wao na umuhimu wake kwani hio ni kuwaongezea mzigo wa masomo watoto.

Katika hatua nyengine, mhe Simai ametoa angalizo kwa wazazi juu ya kutowapa vyombo vya moto watoto wao wanapokwenda Skuli hasa vya maringi mawili kwani vinahatarisha Usalama wao wanapoingia barabarani.

Katika mahafali hiyo, Mhe Simai amewapongeza Wanafunzi waliomaliza masomo yao na kuwataka kuendelea kuzidisha bidii zaidi katika masomo yao katika ngazi zinazofuata ili waweze kufanikiwa katika maisha yao.

Nae Mwalimu mkuu wa Skuli ya FEZA Zanzibar Mr Ali Nunghu Amesema ushirikiano kati ya Skuli hiyo na Wizara ya Elimu Zanzibar, ulianza tokea mwaka 2005, ambao umeweza kuwapa mafanikio mazuri na kufanikiwa kuwa miongoni mwa Skuli bora Tanzanzia katika kufaulisha Wanafunzi.

Pia amewashukuru wazazi kwa kufuata muogozo wa Skuli yao na kufanikiwa kufikia malengo waliyoyakusudia.

Aidha Mr Nunghu amewapongeza Wanafunzi waliohitimu masomo yao hasa wa Elimu ya msingi, na kuwataka kuogeza bidii zaidi ya masomo ili waweze kufaulu vizuri hapo baadae.


Akisoma risala kwa niaba ya Wahitimu Mwanafuzi Ulfat Said amewaahukuru Walimu wao wote kwa juhudi walizozichukua kuwasomesha na kuweza kumaliza Elimu yao ya awali ambapo amewanasihi wanafunzi wenzao kuendelea kujisomea kwa bidii pamoja na kudumisha nidhamu ili waweze kufanikiwa katika masomo yao.

Jumla ya Wanafunzi 114 wamehitimu masomo yao kati ya hao Wanafunzi 69 ni wa kidatu cha NNE na  Wanafunzi 45 ni wa  darasa la sita

No comments:

Post a Comment

Pages