Mratibu wa Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC), Kongani ya Ruvuma, Marcel Mutunda akionesha wanaandishi wa habari miche ya Misaji ambayo itapandwa katika Vijiji vya wilayani Nyasa mkoani hapo.
NA SULEIMAN MSUYA
KATIKA kuhakikisha uhifadhi na utunzaji misitu unakuwa endelevu Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC), kupitia Kongani ya Ruvuma unatarajia kupanda miti ya Misaji 300,000 katika Vijiji vya Liuli, Mkali A, Mkali B na Lipingo wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.
Miche hiyo 300,000 itatolewa na FORVAC kupitia Muungano wa Wakulima wa Miti (TGA) kwenye vijiji hivyo.
Program ya FORVAC ipo kwenye Idara ya Misitu na Nyuki chini ya ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland na Wizara Maliasili na Utalii ya Tanzania.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa FORVAC Kongani ya Ruvuma, Marcel Mutunda wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii.
Mutunda amesema wanatarajia kugawa miche ya Misaji (Teak) 300,000 kwa wanavijiji waliopo kwenye TGA ambao wameonesha utayari ya kupanda miti ya Misaji kibiashara.
Amesema utaratibu wa ugawaji na upandaji miti unatarajiwa kuanza wiki inayoanza kesho hadi mwanzoni mwa mwezi Februari 2021.
Mratibu huyo wa Kongani ya Ruvuma amesema wapo kwenye hatua ya kukamilisha michakato muhimu kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ambao ndio wanawauzia miti hiyo.
"Wiki inayoanza kesho au mapema mwezi Februari 2021 tunatarajia kuanza kugawa na kupanda miti ya Misaji 300,000 kwa TGA za Liuli, Mkali A, Mkali B na Lipingo wilayani Nyasa mkoani hapa," amesema.
Mutunda amesema FORVAC imekuwa ikitoa miche kwa wanavijiji wenye ardhi inayokubali miti ya Misaji ambapo awali walitoa miche 150,000 iliyogharimu shilingi milioni 75 na kwa sasa wanatoa miche 300,000 inayogharimu shilingi milioni 150.
Amesema wameamua kutoa miche hiyo kipindi hiki cha mvua ili iweze kuota kwa haraka na kuwapatia faida wanavijiji hao kwa muda mfupi.
"Miti hii ya Misaji maarufu kama Teak ina soko kubwa duniani pia ni mbadala wa uvunaji haramu kwa miti ya asili kwa ajili ya mbao hivyo tunawashauri wananchi kuipanda ili waitumie kibishara kama tunavyofanya huku Liuli, Mkali A, Mkali B na Lipingo," amesema.
Mwenyekiti wa TGA, Liuli Samweli Mawanja amesema mwaka 2019/2020 walipata ruzuku ya miche 81,150 sawa na hekta 72.1 na kunufaisha wakulima 80 hivyo ni imani yao mwaka huu itaongezeka.
Mawanja amesema FORVAC wameweza kufungua fursa ambayo imepokelewa na wanavijiji wengi na kwamba hawatawaangusha.
"2020/2021 tumeomba FORVAC, miche 300,000 ambayo itapandwa katika vijiji vya Liuli, Mkali A, Mkali B na Lipingo.
Huu ni mradi pekee tangu tupate Uhuru umeweza kustawi kwa kasi kubwa hali ambayo imepokelewa vizuri na wanavijiji," amesema.
Mawanja amesema miti ya misaji ambayo wamepanda itatumika kujenga mitumbwi na maboti na kuachana kukata misitu ya asili.
Mwenyekiti huyo amesema wanatarajia kuondoa umaskini kupitia miti hiyo huku uhifadhi ukiwa wa uhakika.
Ofisa Maliasili wa Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma Bugingo Bugingo amesema katika kuhakikisha misitu inakuwa endelevu wanapaswa kupanda miti 800,000 wilayani humo.
Bugingo amesema wana eneo lenye ukubwa wa hekta 700 ambapo hekta moja inachukuwa miche 1,111 hivyo kwa ukubwa huo wanahitaji miche 800,000 ila wataanza na hiyo 300,000
Amesema kwa sasa wanahitaji miche laki tatu ili kuweza kuihudumia bila shida yoyote ambayo itafanya misitu kuwa endelevu.
"Hitaji letu ni miche 800,000 lakini kwa mwaka huu tunatarajia kupata miche laki tatu au mbili ambazo tutaweza kuihudumia," amesema.
Ofisa Maliasili huyo amesema upandaji wa miche hiyo utachochea uhifadhi na utunzaji wa mazingira ambayo yameanza kuharibiwa lakini pia ni miti ya biashara.
Amesema uamuzi wa FORVAC kuwapatia miche ya kwanza 150,000 na hii ya sasa 300,000 utaweza kufanikisha malengo yao kwa mwaka huu.
Amesema wamekuwa wakigawa miche kwa wanavijiji ambao wapo tayari kupanda baada ya kupata mafunzo na faida yake.
No comments:
Post a Comment