Serikali
kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
imesikitishwa na kitendo askari wa ulinzi (SUMA - JKT) kumpiga ndugu wa
mgonjwa aliefika kumjulia hali mama yake katika Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa wa Shinyanga.
Hayo
yamesemwa leo na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi pindi
akiongea na Maafisa habari wa Wizara ya Afya katika Ofisi za Wizara hiyo
katika jengo la Bima ya Afya Jijini Dodoma.
"Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesikitishwa na
inalaani sana kitendo hicho kilichofanywa na mlinzi wa SUMA - JKT"
amesema Prof. Makubi.
Akielezea
juu ya tukio hilo Prof. Makubi amesema kuwa, Mnamo Januari 22, 2021
Ijumaa jioni askari wa kujenga taifa (SUMA-JKT) alionekana akimpiga
ndugu wa mgonjwa katika maeneo ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Shinyanga jambo ambalo ni kinyume na maadili na taratibu za kazi.
Aidha,
Prof. Makubi amesema kuwa, Wizara kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa
Mkoa wa Shinyanga kupitia Mkuu wa Wilaya imeelekeza mlinzi huyo atolewe
kwenye kituo hicho cha kazi na kurudishwa makao makuu ya kanda ya jeshi
hilo kwaajili ya hatua za kinidhamu kulingana na taratibu za jeshi
hilo.
Hata hivyo, Prof.
Makubi ameeleza kuwa, Katibu Mkuu (Afya) Prof. Mabula Mchembe ameelekeza
kupata maelezo kutoka kwa uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Shinyanga wa jinsi tukio hilo lilivotokea, mazingira yake na hatua
zilizochukuliwa na uongozi wa Hospitali hiyo.
Pia,
ufanyike uchaguzi kama kulikuwa na uzembe wa utekelezaji wa mfumo na
mwongozo wa utoaji huduma kwa mteja (customer care)ambao ulitolewa na
Wizara kwa vituo vyote vya kutolea huduma za Afya ili kuona kama
kulikuwa na udhaifu mpaka tukio hili kutozuilika, huku akisisitiza baada
ya uchunguzi huo hatua stahiki zitachukuliwa.
Mbali
na hayo, Prof. Makubi ametoa rai kwa wananchi kuwa watulivu wakati
hatua zikiendelea kuchukuliwa, huku akiwaasa wananchi kuendelea kupata
huduma za Afya bila wasiwasi kwani Serikali imejipanga kuhakikisha suala
hili halijirudii tena.
"Rai
ya Wizara, tunaomba wananchi wawe watulivu wakati suala hili
linafanyiwa kazi, na Jamii iendelee kupata huduma katika vituo vyote vya
kutolea huduma za Afya nchini bila wasiwasi wowote, kwani Serikali
imejipanga kuhakikisha suala hili halijirudii" amesema Prof. Makubi.
Wakati
huo huo, Prof. Makubi ametoa wito kwa wananchi kufuata na kuzingatia
taratibu zilizowekwa za muda wa kuingia na kuona wagonjwa katika vituo
vyote vya kutolea huduma za Afya nchini.
Pamoja
na hilo, Prof. Makubi amewataka wananchi kutumia vizuri mifumo ya
Mawasiliano ambayo imewekwa sehemu mbali mbali ikiwa ni pamoja na kupiga
namba 199 bila malipo na za viongozi ili kuwasilisha malalamiko ili
kufikia maamuzi sahihi ya migogoro.
Pia,
amewataka Viongozi na Watumishi wote kuendelea kusimamia vizuri huduma
bora za afya kwa wananchi wanaowahudumia, kisha kuwakumbusha kusimamia
vizuri miongozo ya huduma kwa wateja ambayo ilishatolewa na Wizara.
No comments:
Post a Comment