Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, akijibu hoja mbalimbali mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, zilizoulizwa na Kamati hiyo, jijini Dodoma.
NA MWANDISHI WETU
Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA)
umesema kuwa umeongeza mapato yake ya ndani (Own Sources) kutoka Shilingi
Bilioni 4 kwa mwaka wa fedha 2006/07 hadi kufikia Shilingi Bilioni 54 kwa mwaka
wa fedha 2019/20.
Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa TEMESA,
Mhandisi Japhet Maselle, wakati akiwasilisha taarifa kuhusu Muundo na majukumu
ya Wakala huo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu jijini Dodoma.
Mhandisi Maselle, amesema kuwa ongezeko
hilo limeifanya TEMESA Kupunguza utegemezi wake kwa Serikali katika
kujiendesha kwake na kuweza kuchangia Mfuko Mkuu wa Serikali kila mwaka.
“Mfano katika mwaka 2018/19 tulitoa kiasi cha
Shilingi 1,130,209,422.50 na mwaka 2019/20 kiasi cha shilingi
1,224,378,108.24 zilitolewa gawio kwa Serikali", amesema
Mhandisi Maselle.
Aidha, amefafanua kuwa ongezeko hilo
pia limeiwezesha TEMESA kuongeza idadi ya Vivuko kutoka 13 mwaka 2005
hadi kufikia 33 mwaka 2020 vikiwemo Vivuko viwili vipya vilivyokamilika
kujengwa kwa ajili ya kutoa huduma katika Mkoa wa Geita (Chato-Nkome) na Pwani
(Mafia-Nyamisati).
Maselle, ameeleza kuwa mbali na
miradi hiyo TEMESA imeshiriki katika miradi mingine ikiwemo kuweka mifumo ya
umeme na usalama katika miradi mbalimbali ya kimkakati kama vile Mwalimu Julius
Nyerere Dam,
Mkulazi Sugar Industry, Mji wa Serikali Mtumba
na Ukuta wa Mirerani.
Kuhusu ujenzi wa karakana katika kila wilaya, Mhandisi Maselle, amesema kuwa tayari TEMESA imenunua karakana zinazotembea (mobile workshop), kwa karakana ambazo zipo nje ya miji na kukarabti zile zilizochoka ili kurahisisha huduma kwa wateja wao.
"Tunachokiomba kutoka Serikalini ni
kupatiwa fedha kwa wakati ili kuboresha miundombinu ya karakana zetu ili
kuwa na ufanisi katika utengenezaji wa magari", amesisitiza Maselle.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa Suleiman Kakoso, amesema kuwa ili wakala huo uweze kusimama na kujiendesha kibiashara Serikali inatakiwa itoe fedha kwa wakala huo.
Ameiagiza Wizara kupitia TEMESA na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuwasilisha mchanganuo wa madeni wanayodai katika taasisi zote za Serikali kwa Kamati hiyo ili kuweza kusaidia kusukuma na kukumbusha Serikali kulipa madeni hayo.
Ameitaka pia Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT), kuendelea kujikita katika utoaji wa elimu kwa ngazi ya chini ili kupata wataalamu kama mafundi sanifu na mafundi mchundo ambapo kwa sasa wataalamu hao wanaonekana kupungua.
TEMESA, TBA, Vikosi vya Ujenzi pamoja na ICoT ni baadhi ya Taasisi zilizo chini ya Sekta ya Ujenzi ambapo leo zimewasilisha taarifa zao kuhusu miundo na majukumu yao kwa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu ambapo pamoja na mambo mengine Taasisi hizo zimetakiwa kufanya kazi kwa ufanisi na weledi ili kuleta tija kwa Taifa.
No comments:
Post a Comment