HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 19, 2021

Rais Magufuli mgeni rasmi kilele siku ya sheria

Rais wa Tanzania, John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini  yatakayofanyika mkoani Dodoma, Februari Mosi, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Januari, 18 2021, Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema kuwa siku hiyo ya Sheria itatanguliwa na Wiki ya Sheria ambayo ni mahususi kwa ajili ya utoaji wa elimu ya sheria na taratibu za kimahakama kwa wananchi.

Amesema wiki ya Sheria itaanza Januari 23 hadi 29, 2021 katika viwanja vya ‘Nyerere Square’ jijini Dodoma na kuongeza kuwa wiki hiyo itazinduliwa na matembezi maalum.

“Matembezi hayo ambayo yataanzia Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma na kuishia katika Viwanja vya Nyerere Square yatakayofanyika Siku ya Januari 24, 2021, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan,” amesema

Amesema kutakuwa na wiki nzima ya maonesho katika viwanja vya Nyerere Dodoma na kwenye maeneo mbalimbali ya mahakama nchini lakini kilele cha maadhimisho hayo itakuwa Februari Mosi mwaka huu katika viwanja vya Chinangali Dodoma.

“Mgeni rasmi siku hiyo anatarajiwa kuwa Rais Magufuli, hivyo tunaomba wananchi wajitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo kwa sababu kuna mambo mengi watajifunza  na watapata huduma na taratibu za ufunguaji wa mashauri, Sheria na taratibu zinazotumika katika kuendesha mashauri,” amesema

Aidha amesema kuwa maudhui ya maadhimisho haya yanaashiria kuanza rasmi kwa mwaka mpya wa shughuli za Mahakama na yameambatana na miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Mahakama Kuu.

“Kauli mbiu ya maadhimisho hayo inalenga kuonesha maudhui ya kuonesha ufanisi wa utoaji haki katika kipindi cha miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Mahakama Kuu, kwa hiyo kauli mbiu itakuwa ‘Miaka 100 ya Mahakama Kuu, mchango wa mahakama katika kujenga nchi inayozingatia uhuru, haki, udugu, amani, ustawi wa mwananchi kati yam waka 1970 na mwaka 2020,” amesema

Amesema maudhui hayo yanakumbusha mchango wa mahakama ya Tanzania kuanzia enzi za ukoloni mpaka sasa.

Hata hivyo Jaji Mkuu amesema kuwa sheria, utawala wa sheria na mfumo wa utoaji haki kwa wakati ni nyenzo muhimu katika kufanikisha na kurahisisha biashara, uwekezaji, ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.

No comments:

Post a Comment

Pages