HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 25, 2021

TAFORI KUKUTANISHA WANASAYANSI, WATUNGA SERA 300

 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), Dk. Revocatus Mushumbusi akifungua warsha ya mfumo wa utoaji taarifa za uhalifu na uharibifu katika misitu ya mazingira asilia ya milima ya tao la mashariki, iliyofanyika Tarehe 30 Julai, 2020 TAFORI Makao Makuu, Morogoro.

 
 
NA SULEIMAN MSUYA
 

WANASAYANSI, watunga sera, wachakataji, watafiti, wazalishaji na watumiaji wa mazoa ya misitu na nyuki zaidi ya 300 wanatarajiwa kukutana kwenye kongamano la kimataifa la siku tatu kujadili sekta hiyo.

Kongamano hilo la siku tatu limendaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI).

Akizungumzia kongamano hilo Kaimu Mkurugenzi wa TAFORI, Dk.Revocutus Mushumbusi amesema dhumuni ya kuandaa kongamano hilo ni kuhakikisha kada inayojishughulisha na sekta hiyo inaonesha kwa umma inachofanya.

Amesema kongamano hilo linalotarajiwa kufunguliwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan litafanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam kuanzia Februari 23 hadi 25/2021 ambapo kutakuwa na uwasilishaji wa utafiti wa sekta hiyo.

Dk.Mushumbusi amesema kongamano hilo la Kimataifa la Sayansi juu ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu na Nyuki kwa ajili ya maendeleo endelevu ya viwanda ni muhimu kwa taasisi na wadau wake.

"Februari 23 hadi 25,2021 tunatarajia kukutanisha wanasayansi, watafiti, wachakataji, wauzaji, watunga sera na watumiaji wa mazao ya misitu zaidi ya 300 ili kujadili kwa pamoja kuhusu sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya nchi," amesema.

Mushumbusi amesema kongamano hilo litatumika kuonesha utafiti ambao umefanywa na watafiti wa TAFORI na wadau wengine katika sekta hiyo.

Dk.Mushumbusi amesema kukutana kwa kundi hilo kutasaidia kupatikana kwa mawazo chanya ya kuifanya sekta hiyo kuwa endelevu.

Kaimu Mkurugenzi huyo amesema katika kongamano hilo la kimataifa wanatajia kupata wawakilishi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Wizara ya Maliasili na Utalii, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wakala wa Huduma za Misiti Tanzania (TFS), Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC), Vyuo vya Misitu na Nyuki.

Amesema pia wanatarajia kupata wawakilishi kutoka Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA), Shirika la Mpingo Conservation Initiative na mengine mengi.

"Katika kongamano hilo kutakuwa na wawakilishi kutoka nchi ya Finland, Nigeria, Afrika Kusini, Zimbabwe, Kenya na Malawi," amesema.

Aidha Kaimu Mkurugenzi huyo amewataka wananchi mbalimbali kujitokeza katika kongamano hilo kwani kutakuwa na fursa za kibiashara kupitia mazao ya misitu.

Amesema sekta hiyo ikitumiwa vizuri itachochea ukuaji wa viwanda na uhifadhi nchini hivyo dhana ya kukuza uchumi na ajira itafanikiwa.

No comments:

Post a Comment

Pages