Na Eliafile Solla, aliyekuwa Morogoro
KATIBU Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo amemuagiza Mkuu wa chuo cha Ardhi Morogoro kuandika barua kwenda Halmashauri zote za Mkoa wa Morogoro kuona jinsi gani wanaweza kuwatumia wataalam kutoka chuoni hapo kumaliza migogoro ya ardhi inayosababishwa na ujenzi holela na kugombania mipaka ya maeneo.
Kalobelo aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akisoma hotuba kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwenye sherehe za mahafali ya 39 ya Chuo cha ardhi Morogoro ambapo jumla ya wahitimu 394 walitunukiwa vyeti na kati yao 110 walikuwa wa kike, 284 wa kiume na kauli mbiu ya sherehe hizo ilikuwa ni ‘‘Usimamizi bora wa rasilimali za ardhi ni msingi wa maendeleo endelevu na jumuishi.”
‘‘Ni aibu kwa Mkoa wa Morogoro kuendelea kuteseka na Migogoro ya ardhi wakati Chuo kinachozalisha watalaam wa Kupanga na Kupima kipo hapa hapa. Naagiza kabla mwaka huu haujaisha Halmashauri zote za mkoa wa Morogoro ziwe na mpango mkakati kuona jinsi gani ya kushirikiana na Chuo cha Ardhi Morogoro kuhakikisha kila kipande cha ardhi kinapangwa, kupimwa na kumilikishwa, alisema Kalobelo’’.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro. Huruma Lugala alisema, chuo kinao usajili kamili (Full Registration) pamoja na ithibati kamili (Full accreditation) ya Baraza la Taifa la Elimu na Ufundi yaani ‘NACTE’. Usajili huo na ithibati vinatoa uwezo kwa chuo kujipanua kwa kuanzisha kozi mbalimbali zenye tija kwa Taifa na jamii kwa ujumla.
Mbali na kuzalisha wataalam wa Kupanga na Kupima, Chuo cha ardhi Morogoro kimekuwa kikishiriki kutoa huduma ya ushauri wa kitaalamu na kufanya miradi ya urasimishaji ambayo hadi sasa inatekelezwa katika Mikoa ya Dar es salaam, Arusha, Morogoro, Mtwara, Kilimanjaro na Iringa.
No comments:
Post a Comment