Shirika la Kimataifa la Korea (KOICA) limetoa msaada wa mashine tatu za kuchukulia sampuli za maradhi ya Corona (K-Walk Through Booth) ambazo zimewekwa katika vituo vikuu vya kuingilia wageni Zanzibar.
Mkurugenzi
Mkaazi wa Ofisi ya Koica Tanzania Kyucheol Eo amemkabidhi Mkurugenzi
Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Abdalla Salim Ally moja ya mashine hizo
katika sherehe zilizofanyika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani
Karume Kisauni.
Amesema
Koica itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika kuimarisha Mipango yake ya Maendeleo ikiwemo dira ya 2050 na
Mpango Mkakati wa Maendeleo.
Ameongeza
kuwa Sekta ya Afya na Elimu ni kipaumbele cha Koica hivyo msaada wa
vifaa hivyo K-Walk Through Booth ni moja ya juhudi wanazochukua za
kuimarisha afya za wananchi wa Zanzibar.
Dk.
Abdalla amelishukuru Shirika la Koica kwa misaada inayotoa hasa kwenye
sekta ya Afya ambayo imesaidia sana katika mapambano dhidi ya maradhi ya
kuambukiza.
Amesema
Koica walikua wa mwanzo kuisaidia Zanzibar wakati wa kukabiliana na
Kipindupindu miaka michache iliyopita na hadi sasa maradhi hayo yameweza
kudhibitiwa kwa kiasi kikubwa.
Amewashauri wafanyakazi watakaosimamia mashine hizo kuwa na uangilizi nzuri na kuzitunza ili zidumu kwa kipindi kirefu.
Akielezea
ufanisi wa mashine za K-Walk Through Booth, Mkurugenzi Kinga na Elimu
ya Afya Dk. Fadhil Abdalla amesema zitarahisisha kuchukuwa sampuli za
wasafiri kwa muda mfupi na kuondosha usumbufu na msongamano uliokuwepo.
Alisema baada kuchukua Sampuli zitakazobainika kuwa na mashaka zitapelekwa maabara kwa uchunguzi zaidi.
Mashine
za K-Walk Through zimewekwa Uwanja wa Ndege wa Kimatiafa wa Abeidi
Amani Karume Kisauni, Bandari Kuu ya Malindi na Uwamja wa ndege wa
Kisiwani Pemba.
No comments:
Post a Comment