Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Protabas Katambi akikagua banda la Epidemic Control (EPIC) wakati wa Mkutano wa Mwaka wa wadau wanaotekeleza Afua za VVU na UKIMWI zinazowalenga wasichana Balehe na Wanawake Vijana unaofanyika leo April 29 jijini Dodoma.
Na Raymond Mushumbusi WAMJW Dodoma
Naibu Waziri,
Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira
Mhe. Patrobas Katambi, amesema kuwa utafiti unaonesha katika watu 72,000
wanaopata maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kwa mwaka asilimia 40
ni vijana na kati ya hao asilimia 80 ni wasichana wenye umri kati ya
miaka 15-24.
Hayo
ameyasema leo April 29,2021 akifungua mkutano wa mwaka wa wadau
unaotekeleza afua za VVU na Ukimwi zinazowalenga wasichana balehe na
wanawake vijana unaofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma.
Mhe.Katambi
amesema kuwa Katika utafiti huo watu 72,000 wanapata maambukizi mapya
kwa mwaka na kati yao 40% ni vijana; kati ya hao vijana 80% ni wasichana
wa umri wa miaka 15 – 24 ikimaanisha kuwa kila kundi la vijana 10
wenye maambukizi 8 kati yao ni vijana wa kike na 2 ni vijana wa kiume.
''Ni
muhimu kuwahimiza vijana na watu wote kupima ili kujua hali zao,
kutumia dawa kwa waliogundulika na VVU na kuepuka maambukizi ikiwa bado
hawajapata maambukizi''amesema Katambi
Aidha,
Katambi amesema kupitia matokeo ya utafiti wa 2016/17 Serikali iliona
umuhimu wa kufanya jitahada za pamoja na wadau katika mapambano dhidi ya
VVU na UKIMWI, hususani katika kundi la vijana wa kike.
“
Nimeelezwa kuwa kuna juhudi zinazofanywa kupitia miradi ya DREAMS
initiatives wenye lengo la kuwafikia mabinti balehe na wanawake vijana
wenye umri wa miaka 15 - 24 wakiwemo waliozaa kwenye umri mdogo,
wanaoishi na maambukizi ya VVU, wenye mahusiano na mpenzi zaidi ya
mmoja, walioolewa katika umri mdogo, mabinti waliocha shule, na mabinti
wanaoongoza kaya katika jamii na walio ndani ya shule”amesisitiza
Katambi.
Hata hivyo
Katambi amesema kiwango cha ushamili kimeendelea kupungua sambamba na
kiwango cha maambukizi mapya na vifo vitokanavyo na ukimwi.
Amesema
wastani wa kitaifa wa ushamili wa VVU ni asilimia 4.7 ambapo mkoa wa
Njombe umekuwa kinara kwa kuwa na asilimia 11.4 ukifuatiwa na Mikoa ya
Iringa asilimia 11.3,Mbeya asilimia 9.3 na Mkoa wa Dodoma maambukizi
yameongezeka kutoka asilimia 2.9 hadi kufikia asilimia 5.
Pia
Katambi ametaja miradi inayolenga kutoa elimu ya kujikinga na VVU
kuwa ni pamoja na mradi wa DREAMS unaotekelezwa katika Mikoa 4
Halmashauri (12), Mradi wa Ujana Salama unatekelezwa katika Mikoa 4 na
Halmashauri (11) na mradi wa Timiza Malengo unatekelezwa Katika Mikoa 5
na Halmashuri (18).
Katambi
amesema kuwa '' Niwambie Serikali itaendelea kushirikiana na wadau
mbalimbali kutekeleza miradi ya maendeleo inayolenga kuwalinda Wasichana
Balehe na Wanawake Vijana na vijana kwa jumla kwa kuimarisha utoaji wa
huduma za afya na kijamii hususani kwenye kupunguza maambukizi ya VVU
hasa kwa vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa''amesema Katambi
Hata
hivyo Katambi amesema kuwa malengo ya nchi ni kufikia sifuri ya
maambukizi mapya ya VVU, sifuri ya ubaguzi na unyanyapaa utokaonao na
UKIMWI na sifuri ya vifo vitokanavyo na UKIMWI ifikapo 2030.
Kwa
upande wake,Mkurugenzi Mkuu Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania
(TACAIDS),Dk.Leonard Maboko amesema kuwa lengo la kikao hicho ni
kuwaleta wadau na kuona wamefikia wapi na wamekutana na changamoto zipi
pamoja na kuzitatua.
"Sisi
TACAIDS kazi yetu ni kuratibu na ndio maana hapa kuna taasisi kazi yetu
kubwa ya hili kundi ni kuratibu kila mwaka hivyo hichi kikao ni cha
kuwaleta hawa wadau kuona wamefikia wapi na wamekutana na changamoto
zipi pamoja na kuzitatua,ili kujadiliana tulipotoka tulipo na
tunapoelekea,"amesema Maboko.
Dkt.Maboko
amesema kuwa Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa aliagiza Tacaids ifanye kazi
na vijana ambapo alidai kwa sasa wanafanya kazi nao hususan wasanii.
Hata hivyo Dkt.Maboko amesema kuwa takwimu zinaonesha vijana ni kundi lenye Changamoto katika maambukizi ya Ukimwi.
"Tulianzisha
Kijiji Maalum kwa vijana ambayo inalenga masuala ya vijana na haya yote
yalikuwa ni maagizo ya Waziri Mkuu na yalitokana na
"Maambukizi
mapya asilimia 40 yalikuwa yanatokea kwa vijana lakini asilimia 80 ya
hao vijana ni wa kike,kwa umaalumu kabisa ndio maana hili kundi likapewa
msisitizo huu.Takwimu zilituonesha hivyo tukaona kuna haja ya kuweka
mkazo katika hili,"amesema
Awali
,Balozi Mwakilishi wa wasichana balehe na wanawake vijana Rosemari
Shani akisoma risala amesema kuwa wanakabiliwa na changamoto za upungufu
wa vituo vya kutolea huduma kwa vijana,ukosefu wa soko la uhakika wa
bidhaa wanazozalisha,uelewa mdogo wa jamii kuhusu kinga za VVU.
"Elimu
zaidi iendelee kutolewa tunaomba uziimize Halmashauri ziendelee kutoa
mikopo kwa wanawake.Sisi Kama wasichana tunakuahidi kufanya juhudi
kujiunga na Veta na Sido ili kukuza ujuzi.Tutaendelea kuwajibika katika
familia zetu,"amesema .
Hata
hivyo amesema kuwa wanajivunia kumpata Rais mwanamke,Samia Suluhu
Hassan kwani hiyo ni chachu kubwa kwao kuendelea kusoma na kufanya kazi
kwa bidii.
"Tunajivunia
kumpata Rais mwanamke jambo hili ni chachu kubwa kwetu.Tunaishukuru
Serikali na wadau ambao wanatusaidia tunatarajia mambo mazuri,"amesema
No comments:
Post a Comment