Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Emmanuel Tutuba (kulia) na Balozi wa China, Wan Ke (kushoto), wakisaini Mkataba wa msaada wa kiasi cha Sh. Bilioni 35.37 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini, Jijini Dar es Salaam.
NA BENNY MWAIPAJA, DAR ES SALAAM
SERIKALI
ya China imeipatia Tanzania msaada wa yuan za China milioni 100 sawa na
Sh.Bilioni 35.37 utakaotumika kutekeleza miradi itakayokubaliwa ama
kuridhiwa na pande zote mbili.
Mkataba
wa makubaliano ya msaada huo umesainiwa Jijini Dar es Salaam na Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba, kwa niaba ya Serikali
ya Tanzania na Balozi wa China nchini Tanzania Wan Ke, kwa niaba ya
Serikali ya China.
Akizungumza
wakati wa kusainiwa kwa Mkataba huo, Tutuba alipendekeza msaada huo
utumike kupanua ujenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, kupandisha
hadhi Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kuwa Chuo Kikuu, kutekelea
mradi wa uhifadhi wa Miamba katika eneo la Ngorongoro (Geopark), na
miradi mingine itakayoafikiwa na Serikali zote mbili.
Aidha,
aliishukuru China kwa misaada na mikopo yenye masharti nafuu
inayoipatia Tanzania kuanzia mwaka 2010 na kutumika kujenga miundombinu
ya Reli, Elimu, Afya, Tehama, Nishati, Maji, Sekta ya Viwanda, Kilimo,
Usalama, na Misaada ya Kitaalam, iliyofikia dola za Marekani bilioni 1.8
sawa na Sh.Trilioni 4.15.
“Nachukua
fursa hii kukuhakikishia kwamba, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania itachukua hatua zote muhimu kuhakikisha kwamba miradi
itakayotekelezwa kwa fedha za msaada huu inakamilika kwa wakati ili
kufikia malengo yaliyokusudiwa” aliongeza Tutuba.
Kwa
upande wake Balozi wa China hapa nchini, Wan Ke, alisema, kuwa msaada
huo ni matokeo ya ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi,
aliyoifanya Januari mwaka huu na ni mwendelezo wa ushirikiano mwema kati
ya China na Tanzania uliodumu kwa zaidi ya miaka 57 sasa.
“Tangu
wakati huo China imeisaidia Tanzania kutekeleza miradi mbalimbali ya
kiuchumi na kijamii ikiwemo ujenzi wa reli ya TAZARA, Uwanja wa Michezo
wa Benjamin Mkapa, Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius
Nyerere(JNCC), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, na Maktaba ya Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam” alisema Balozi Wan Ke.
Alibainisha
miradi mingine iliyofadhiliwa na China kuwa ni upanuzi wa Chuo cha
Polisi Moshi mkoani Kilimanjaro, Ujenzi wa Ofisi ya Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dar es Salaam ambapo
miradi hiyo yote imekabidhiwa Serikali ya Tanzania.
“Vile
vile tumewaleta madaktari wa kujitolea wapato 25 ambao wamekuwa
wakijihusisha na utoaji wa tiba ya moyo na kupambana na malaria maeneo
mbalimbali nchini na hivi sasa pia China imefadhili ujenzi wa Chuo cha
Ufundi Stadi mkoani Kagera ambacho ujenzi wake ukikamilika kitakuwa chuo
kikubwa kuwahi kujengwa hapa nchini.
Aidha,
Wan Ke, alisema kuwa China imeipatia Tanzania msaada wenye thamani ya
dola za Marekani milioni 1.3 kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa
COVID-19 kwa ajili ya kununulia barakoa, vitakasa mikono, vifaa tiba na
dawa na kwamba nchi yake imetia saini kushiriki kwenye mpango wa
kuahirisha ulipaji wa madeni (DSSI) ili kuruhusu Serikali kuelekeza
fedha hizo kwenye maeneo mengine katika kupambana na maradhi hayo
yanayoendelea kuitikisa dunia.
Akizungumzia
kuhusu uwekezaji wa China hapa nchini, Balozi Wan Ke, alisema kuwa
licha ya kuwepo kwa ugonjwa wa COVD-19 na kuathiri uchumi wa nchi zote
mbili, katika mwaka 2020, biashara na uwekezaji ulifikia dola milioni
4.58 sawa na ongezeko la asilimia 9.9.
“Uwekezaji
wa mitaji wa China nchini Tanzania umefikia dola za Marekani milioni
159.71 ikiwa ni ongezeko la asilimia 62.37 na kwa kipindi cha robo ya
kwanza ya mwaka huu kiwango cha biashara kimekua kwa asilimia 59.71
ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka uliopita 2020 huku bidhaa
kubwa zinazoingia katika soko la China hivi sasa ni muhogo, mvinyo, na
maharage ya soya,” alisema Ke.
Balozi
Wan Ke, alisema kuwa anaimani na uongozi wa Rais, Samia Suluhu Hassan,
ambaye ameahidi kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini pamoja
na kulinda uwekezaji ili kuwaongezea kujiamini zaidi na kwamba uamuzi
huo unaungwa mkono na kampuni za China zilizowekeza hapa nchini na
utawavuta wawekezaji wengi zaidi kutoka China kuja kuwekeza mitaji na
teknolojia hapa nchini.
No comments:
Post a Comment