Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dk. Mwigulu Nchemba (Mb) akiongoza Mkutano kati yake na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb) na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja (Mb), ambao pia uliwakutanisha Wataalamu kutoka Wizara hizo, jijini Dodoma.
NA BENNY MWAIPAJA, DODOMA
WAZIRI
wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, ameishauri Wizara ya Mifugo
na Uvuvi, kusimamia kikamilifu sekta ya mifugo kwa kubuni njia
mbalimbali zitakazoongeza tija katika sekta hiyo.
Dk.
Nchemba ametoa ushauri huo Jijini Dodoma, alipokutana na kufanya
mazungumzo na uongozi wa Wizara hiyo pamoja na Wizara ya Maliasili na
Utalii, kujadili masuala mbalimbali yanayohusu namna ya kuboresha sekta
ya mifugo ili iweze kuongeza mchango katika ukuaji wa uchumi wa nchi na
maendeleo ya watu.
“Tutakavyo
weka mipango ya kisasa ya kukuza uzalishaji katika eneo hili la mifugo,
tutatengeneza wigo mkubwa wa walipakodi, tutabadilisha maisha ya watu
wetu, tutakuza uchumi na ajira,” alisema.
Dk. Nchemba alisema,
kuwa maendeleo ya sekta ya viwanda yanayokwenda kwa kasi hapa nchini
yanahitaji malighafi za kulisha viwanda hivyo na kwamba fursa zilizopo
kwenye sekta ya mifugo ni kubwa na kushauri mbinu za kisasa za
kuendeleza ufugaji ziwekwe bayana na kufanyiwa kazi ipasavyo.
Alisema
utaratibu wa sasa wa wafugaji kuhamahama na mifugo kwa ajili ya
kutafuta malisho na maji umepitwa na wakati na kuahidi kuwa Wizara yake
iko tayari kutoa ushirikiano ili kufanikisha mipango ya kuendeleza sekta
ya mifugo nchini.
Kwa
upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki, alimshukuru Dk.
Nchemba kwa kukutana na viongozi wa Wizara hizo mbili na kuahidi kuwa
ushauri uliotolewa utafanyiwa kazi kikamilifu ambapo ameunda timu ya
wataalamu kwa ajili ya kuchambua mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa
katika kikao hicho alichosema kilikuwa ni cha muhimu.
“Tutaangalia
namna ya kupanua na kuwa na maeneo maalum ya malisho ya mifugo yetu
pamoja na kuboresha ufugaji ili ubadilike kutoka ufugaji wa kiasili
kwenda ufugaji wa kisasa ili kuongeza tija,” alifafanua.
Ndaki alisema,
kuwa wafugaji watakaokuwa tayari kubadilisha namna ya ufugaji wao
watapelekwa kwenye maeneo hayo yatakayowekewa miundombinu yote muhimu ya
ufugaji ikiwemo maji na majani ya malisho.
Wakizungumza
katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel
Tutuba, aliishauri Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuanzisha maeneo ya
ufugaji (Ranch) kila mkoa na kujenga miundombinu itakayowasaidia
wafugaji kufuga mifugo yao kisasa ili waweze kuongeza kipato chao,
kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi na kuondokana na umasikini.
Naye
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Elisante Ole-Gabriel
aliiomba, Wizara ya Fedha na Mipango kuiwezesha Wizara yake kifedha kwa
ajili kufanya utafiti katika sekta ya mifugo ili kuongeza mbinu za
kisasa za kuongeza uzalishaji.
Naye
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dk. Allan Kijazi,
alishauri kuwa ili sekta ya mifugo iweze kupiga hatua kubwa kuna umuhimu
wa kutafuta masoko kwa ajili ya bidhaa za mifugo, kuongeza elimu kwa
wafugaji, pamoja na kuwa na maeneo ya kimkakati ya viwanda vya kuchakata
bidhaa za mifugo ni muhimu likafanyiwa kazi.
Kwa
mujibu wa takwimu zilizotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na
Uvuvi (Mifugo), kwenye kikao hicho Prof. Ole-Gabriel, Tanzania ni ya
pili kwa kuwa na mifugo mingi barani Afrika kwa kuwa na ng’ombe milioni
33.4, mbuzi milioni 21.29, Kondoo milioni 5.65, Punda 657,380, lakini
tija yake bado ni ndogo.
No comments:
Post a Comment