HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 09, 2021

KUSUASUA MIRADI YA MAJI MKUU WA WILAYA YA MULEBA ATOA NENO

 


Mkuu wa wilaya ya Muleba mhandisi Richard Luyango.

 

Na Lydia  Lugakila, Muleba

Mkuu wa Wilaya ya Muleba mkoani Kagera Mhandisi Richard Luyango ametoa siku 5 kwa baadhi ya madiwani wilayani humo pamoja na  watendaji wa halmashauri kukutana ili kujua  kwanini  wameshindwa kukamilisha baadhi ya miradi ikiwemo ya maji agizo lililotolewa na naibu waziri wa maji.

Mkuu wa wilaya ya Muleba mhandisi Luyango ametoa agizo hilo katika kikao cha baraza la madiwani kilichojadili masuala mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri hiyo.

Mhandisi Luyango amesikitishwa na baadhi ya madiwani ambao katika kata zao wameshindwa kusimamia miradi ikiwemo ya maji ikiwa ni agizo la naibu waziri wa maji mhandisi Maryprisca Mahundi alilolitoa baada ya kufanya ziara katika baadhi ya kata wilayani humo lililoelekeza mradi wa maji katika kata ya Nshamba kukamilika mapema na kukabidhiwa mnamo Aprili 30 mwaka huu.

" Naibu waziri aliagiza mradi kukamilika mapema leo tupo mwezi Mei, diwani upo watendaji mpo, mamlaka upande wa  maji mpo lakini hamtekelezi ipasavyo, kumbuka  tija  ya mradi ya serikali ni kukamilika na wananchi kuendelea kupata huduma, hivyo basi kupitia kikao hiki ifikapo mei 11, 2021 diwani wa kata ya Nshamba Gozibert Masilingi, diwani  watendaji wa halmashauri tukutane ili kujua kwa nini agizo la naibu waziri halijatekelezwa alisema mkuu huyo wa wilaya".

Ameutaja pia mradi wa maji katika kata ya kamachumu kutokamilika na kuwahimiza viongozi hao akiwemo mwenyekiti wa halmashauri na kamati yake  kwenda kata kwa kata kukagua miradi hiyo na kujenga mazoea ya kupeana taarifa kujua miradi ambayo haijakamilika katika maeneo yao ili kuisaidia serikali.

Aidha ameongeza kuwa miradi ya elimu fedha ilitolewa ambapo ilifanyika harambee kupitia waziri wa elimu katika shule ya msingi na sekondari kaigara na mradi haukukamilika licha ya wananchi na serikali kutoa fedha jambo lililompelekea kutaka majibu ya wapi wamekwama.

Hata hivyo amewahimiza  viongozi hao kukamilisha miradi ya maendeleo katika maeneo yao ikiwemo elimu, maji na barabara pia kusimamia miradi hiyo huku akiwapongeza watendaji hao kwa kuendelea kutekeleza wajibu katika shughuli mbali mbali katika wilaya hiyo ambapo katika makusanyo katika wilaya  hiyo imefikia  asilimia 76 kwa mwaka 2019/2020 huku matarajio yakiwa ni kufikia asilimia 85.

No comments:

Post a Comment

Pages