Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akimkabidhi zawadi mshindi wa kwanza wa KM 42 Wanawake Bi.Monica Cheluto kutoka Kenya katika mbio za Tulia Marathon zinazodhaminiwa na Mhe. Tulia Ackson Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilizofanyika Mei 08, 2021 Jijini Mbeya.
Na Shamimu Nyaki-WHUSM, Mbeya
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Pauline Gekul amezitaka Halmashauri zote nchini kusimamia michezo kuanzia ngazi za vijiji ili wananchi waweze kuimarisha afya zao na kukuza michezo kuanzia ngazi ya chini hadi Taifa.
Mhe. Gekul ametoa maagizo hayo Mei 08, 2021 Jijijini Mbeya akiwa Mgeni Rasmi katika Mbio za Tulia Marathon zinazodhaminiwa na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson.
"Nafahamu kuna asilimia 40 inayotengwa na Halmashauri kwa ajili ya shughuli za maendeleo, natoa rai kwa viongozi wa Halmashauri kutenga fedha kidogo kwenye hiyo asilimia ambazo zitawezesha shughuli za michezo kwenye maeneo yenu kuanzia ngazi za chini kabisa kwenye vitongoji", amesisitiza Mhe. Gekul.
Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Dkt. Tulia Ackson amesema lengo la mashindano hayo ni kuboresha Miondombinu ya Elimu na Afya kupitia Taasisi ya TuliaTrust Fund kwenye Jimbo hilo ambapo zinatarajiwa kufikia Watanzania wengi hapo baadae.
"Tulia Trust Fund ipo kwa ajili ya kusadia na kuwezesha wananchi kiuchumi,tangu mwaka 2018 taasisi hii imesadia wananchi kupitia miradi mbalimbali ikiwemo kuboresha madarasa, mabweni na upatikanaji wa maji na kazi inaendelea" amesema Mhe.Tulia
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Riadha Nchini Filbert Bay amempongeza Naibu Spika huyo kwa kuanzisha mashindano hayo ya riadha.
Mbio hizo zinajumuisha mbio za ndani na nje ya uwanja ambapo kwa hapa nchini zimefanyika kwa mara ya kwanza.
Naye Mshiriki aliyeshika nafasi ya tatu katika mbio za KM 21 ambaye pia ni miongoni mwa Timu ya Taifa ya Riadha inayowakilisha nchi katika mashindano ya Riadha yatakayofanyika baadae mwaka huu nchini Japan, Bw. Alphonce Simbu amesema mashindano hayo yamemsadia kufanya mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya mashindano yajayo ya Kimataifa ambapo ameahidi kufanya vizuri na kuitangaza nchi.
Mbio hizo hufanyika kila mwaka ambapo kwa mwaka huu zimegawanyika katika makundi ya KM 42 na 21 kwa wanaume na wanawake, Mbio za ndani ya Uwanja kwa Mita 100, 200, 400, 800 na 1500 ambapo pia Viongozi na Waheshimwa Wabunge wameshiriki.
No comments:
Post a Comment