HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 22, 2021

Bwege ataka mikutano ya hadhara ianze upyaa


Na Mwandishi Wetu

Aliyekuwa Mbunge wa Kilwa Kaskazini kupitia CUF, Suleiman Bungara maarufu 'Bwege' ameshauri wanasiasa kuanza kufanya mikutano ya hadhara ya kisiasa kwakuwa ni takwa la kikatiba.

Bwege ambaye sasa ni mwanachama kindaki ndaki wa chama cha ACT-Wazalendo ametoa ushauri huo jana Juni 21, 2021 katika mkutano wa ndani wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Othman Masoud Othman.

Bwege alisema Serikali ya awamu ya tano ilikiuka Katiba kwa kuzuia mikutano ya hadhara kwa wanasiasa, hivyo hatarajii kama Rais Samia ataendeleza ukikwaji huo wa Katiba uliofanywa na mtangulizi wake, Rais John Magufuli.

"Nadhani sisi ACT Wazalendo kuanzia sasa tuanze kutoa taarifa kwa polisi tuone kama ubabe huo unaendelea. Tunataka kuona kama Mama atazuia ama ataachia..." alisema.

Aidha Bwege ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Kilwa Kaskazini kwa vipindi viwili mfululizo pia alizungumzia umuhimu wa wanasiasa kuanza kupigania Katiba Mpya.

Alisema hatarajii suala hilo kukwamishwa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais Mwinyi kwakuwa katika kipindi kifipi walichokaa madarakani wameonesha hawataki dhuluma bali wanaamini kwenye haki.

"Tumemsikia Rais Samia Suluhu anasema hataki dhuluma, tumeona pia Mashekhe amewaachia, tunashukuru, lakini  tunasema kikubwa zaidi kwetu sasa aseme na kuhusu Katiba Mpya, lakini kama hakuruhusu Katiba mpya basi tutarudi kwenye nginja ngija' alisema Bwege.


No comments:

Post a Comment

Pages