Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala, akiwa katika ziara ya kukagua Miradi
ya Kimkakati (DMDP) iliyopo wilayani Temeke.
Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala amefanya ziara ya kukagua Miradi
ya Kimkakati ( DMDP) iliyopo wilayani Temeke na kuwataka Wakandarasi
waliokabidhiwa miradi hiyo kutekeleza makubaliano walioingia kwa
kuikamilisha kwa wakati uliopangwa kwani watakaoshindwa hawatapewa
miradi mingine.
Katika ziara hiyo RC Makala
amekagua Mradi wa Barabara ya Mwele iliyopo Kata ya Mbagala, Barabara
ya Kliniki, pamoja Barabara ya Nzasa kupitia Buza hadi Kilungule katika
Kata ya Kilungule yenye gharama ya Sh Bilioni 19.1.
RC
Makala amesema miradi yote ya DMDP itafanyiwa tathmini na wakandarasi
watakaobainika kushindwa kukidhi matakwa yaliyopo kwenye mikataba
waliyoingia na Serikali hawatapewa miradi ya awamu nyingine.
Akiwa
katika Kata ya Kilungule RC Makala alimuagiza mkandarasi aliyekabidhiwa
barabara hiyo kufanya kazi katika muda uliopanga la sivyo akishindwa
hatopewa miradi mingine ya kimakakati.
Amebainisha
kuwa mkandarasi mwenye dhamana ya barabara hiyo atumie busara na
ubinadamu kwa kuwapangishia wananchi waliopo karibu na ujenzi wa
barabara kwao wengi wameathirika na vumbi na udongo ulioingia majumbani
mwao.
Ameongeza kuwa wananchi waendelee kutoa
ushirikiano kwa wakandarasi kwa kufikia mwafaka kabla hawajapangiwa
vyumba maeneo mengine na kwamba madhara yakiongezeka eneo itabidi
walipwe fidia.
RC huyo amesema tayari Seriakali
imetoa Sh bilioni 5 katika ujenzi wa barabara ya Kliniki hivyo
Kampuni ya JASCO iendelee na ujenzi huku kiasi cha fedha kilichobaki
kikiendelea kushughulikiwa.
Kwa upande wake
Mkuu wa Wilaya hiyo Godwin Gondwe amesema maelekezo yote yaliyotolewa na
RC Makala yatatekelezwa ili kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa
wakati.
Aidha, amesema Serikali imetoa Sh
Bilioni 216.7 na kwamba hadi sasa Sh Bilioni 165.3 zimeshalipwa kwa
wakandarasi huku akisisitiza miradi hiyo ikikamilika itasaidia kupunguza
msongamano katika Barabara ya Kilwa.
Naye
Diwani wa Kata ya Kilungule Said Fella ameishukuru Serikali kwa kutoa
fedha za mradi wa barabara unaopita katika kata yake kwani utasadia
kutoa ahueni ya msongamano wa magari kwa wananchi wanaokwenda Chamazi.
No comments:
Post a Comment