HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 19, 2021

TAMWA-ZNZ YAWAFUNDA WAZAZI, WALEZI SIKU YA MTOTO WA AFRIKA

 


Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ Dkt, Mzuri Issa akisisitiza jambo katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Africa yaliofanywa na baadhi ya Asasi za kirai visiwani hapa katika ukumbi wa Haile Salasi mjini Unguja. 
 

Baadhi ya washiriki waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika wakifuatilia mkutano huo.
 
 
Na Talib Ussi, Zanzibar

 

Wakati tukiwa tunaadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA-ZNZ), Dkt. Mzuri Issa, amesema  kuna haja ya wazazi na walezi kubadili mitazamo ya maisha na kutowaamini watu  wasiowajua kwa lengo la kuwaepusha watoto wao na majanga mbalimbali, yakiwemo ya udhalilishaji wa kijinsia.

 

Aliyasema hayo katika ukumbu wa Skuli ya Haile Salasi mjini Unguja katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Africa yalioadhimishwa na taasisi mbali mbali zisizokua za kiserikali mjini hapa.

 

Alisema licha ya uwepo wa matatizo hayo hatarisha kwa watoto lakini hadi leo wapo miongoni mwa wazazi kwenye familia hawana utaratibu wa kuwalinda watoto wao wala kuwafaitilia nyenendo zao na ndio maana baadhi ya watu wengine hutumia mwanya huo kuwafanyia maovu watoto wadogo.

 

Alisema wazazi wana wajibu wa kuwafahamisha watoto wao kukataa kuitikia wito au hata kupanda kwenye chombo chochote cha usari kutoka kwa mtu wasiemjua.

 

''Hivi karibuni tu tumepokea taarifa kuna mtoto aliefanyiwa udhalilishaji na mtu aliempakia kwenye pikipikia ambapo mtu huyo awali alimuita mtoto huyo na kumpakiza kisha kumpeleka anapotaka yeye lakini kwa bahari nzuri raia wema walimuokoa mtoto huyo hatimae muhusika kudhibitiwa''aliongezea.

 

Katika hatua nyengine Mkurugenzi huyo alizitaka mamlaka zinojihusisha na kesi za udhalilishaji kutotumia kigenzo cha ushahidi wa mtoto anaposema aliemfanyia kitendo cha kumdhalilisha kimaumbile ni mpenzi wake licha ya kuwa msichana huyo bado hajatimiza umri wa miaka 18.

 

Alisema kikawaida msichana asietimiza umri wa mika 18 hata kama amejaliwa maumbile makubwa haweza kufanya kitu bila ya kushawishiwa na mwanaume na inapotokea amefanya na kukiri kuwa kafanya kwa ridhaa yake Mahakimu hawapaswi kuchukua kauli hio kama sehemu ya kumuachia mtuhumiwa wa udhalilishaji.

 

Akisoma risala kwa niaba ya watoto wenzake Salma Abeid alisema wakati wakiwa wanaadhimisha siku hio adhimu kwao bado kuna changamoto mbali mbali zinaendelea kuwakabili.

 

Akitaja changamoto hizo ni pamoja na uwepo wa ndoa za umri mdogo na kulazimishwa kazi zisizolingana na umri hatimae kuwadumaza kiakili.

 

Pia alisema suala la udhalilishaji wa kijinsia ni jambo linalowapa wakati mgumu watoto wengi na wapo waliofanyiwa matendo hayo kubaki na kusononeka daima huku wakishindwa hata kurudi skuli.

 

Alieleza kuwa wao kama watoto wa Africa wana ndoto nyingi zinazohitaji kuendelezwa kutoka kwa wazazi wao na jamii kwa ujumla na sio kudumazwa kwa maslahi ya wachache.

 

Awali akisoma ripoti ya utafiti mdogo uliofanywa na TAMWA-ZNZ Meneja miradi wa Chama hicho Ally Mhamed alisema utafiti huo umebaini uwepo wa kasoro mbali mbali katika vyombo vinavojihusisha na mapambano katika kesi za udhalilishaji.

 

Alitolea mfano uhaba wa usafiri katika vituo vingi vya polisi Zanzibar ni tatizo linalosababisha maafisa wa jeshi hilo kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa haraka pale wanapopata taarifa za kutokea kwa matukio katika maeno tofauti.

 

Pia Meneja huyo ameleza uhaba wa vitendea kazi na sehemu za kuskiliza kesi za udhalilishaji katika mahakama mbali mbali visiwani hapa na kupelekea mlundikano mkubwa wa kesi hizo katika mahakama tofauti.

 

No comments:

Post a Comment

Pages